💯KCM2324050; Fanya.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#JumatatuYaMalengo
Mwanamafanikio,
Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.
Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

💯 Neno la leo; Fanya.
Leo ikiwa ni #JumatatuYaMalengo tunaona jinsi ambavyo unapaswa kufanya vitu unavyodhani huwezi kufanya.
Ili upate mafanikio makubwa kwenye maisha yako, lazima ufanye vitu ambavyo hujawahi kufanya, vitu ambavyo wengine pia hawawezi kufanya.
Unaposikia kauli kama hiyo, kitu cha kwanza unachofikiri ni haiwezekani. Na hapo sasa ndiyo unapaswa kuhakikisha unafanya.
Chochote ambacho unaona unapaswa kukifanya, ila unajiambia huwezi kufanya, hicho ndiyo unalazimika kufanya.
Hiyo ni kwa sababu hapo ndipo unapokuwa umeweka breki zinazokuzuia kufanikiwa.
Unapofanya, unakuwa umeachilia breki na kuweza kufanya makubwa kuliko ambavyo umekuwa unafanya.
Umejijengea gereza lako mwenyewe kwa kujiambia ni vitu gani unaweza kufanya na vitu gani huwezi kufanya.
Lakini ukweli ni kwamba kwa uwezo mkubwa uliopo ndani yako, unaweza kufanya chochote unachotaka kufanya.
Zingatia ni kufanya chochote unachotaka na siyo kufanya kila kitu.
Maana hapo ndipo wengi huwa wanachanganya, wanafikiri kwa sababu wanaweza kufanya chochote, basi wanaweza kufanya kila kitu.
Kwa chochote unachotaka kufanya na kujiambia huwezi, hicho ndiyo unachopaswa kufanya, maana ndiyo chenye mafanikio yako makubwa.
Na unachohitaji kufanya ni kuweka malengo kwenye kitu hicho, kisha hatua za kuchukua na kuchukua hatua hizo.
Ukiulizwa swali, unawezaje kumla tembo? Kama utafikiria kumla tembo mzima mzima, kwa hakika haitawezekana.
Lakini ukifikiria kumla kwa vipande vipande, hilo linawezekana kabisa.
Chochote unachojiambia huwezi kufanya ni kwa sababu unakiangalia kwa ukubwa wake na kukata tamaa, kuona hakiwezekani. Lakini ukikigawa kwa kipande, unaona hatua za kuchukua na hatimaye kukipata.
Malengo ndiyo njia ya kugawa kitu chochote kwenye vipande ambavyo unaweza kuvifanyia kazi na kuvifikia.
Kwa chochote unachotaka, weka malengo na mipango kisha anza kufanyia kazi. Hatua kwa hatua utaweza kupata chochote unachotaka, kama utaendelea kufanya kwa msimamo bila kuacha.
💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MJASIRIAMALI MJANJA na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu hatari ya mafanikio. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/12/18/3274
Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kufanya kile ambacho umekuwa unajiambia huwezi kufanya kwa kuweka malengo na mipango kisha kuchukua hatua kwa msimamo bila kuacha.
Kocha.
💯