3276; Siyo kufanya, bali kuacha.

Tim Grover alikuwa Kocha wa aliyewahi kuwa mchezaji bora wa mpira wa kikapu, Kobe Brayant.
Alikuwa pia Kocha wa wachezaji wengine bora kama Michal Jordan na wengineo.
Kazi yake kubwa imekuwa ni kuwajengea wachezaji mtazamo sahihi wa ushindi.

Hapa kuna swala la wachezaji bora sana, ambao walikuwa namba moja dunia nzima kwenye michezo yao kwa nyakati mbalimbali, kuwa na makocha hata kipindi ambacho walikuwa kileleni. Hilo siyo somo la leo, ila sitaki likupite, ni muhimu sana kila anayetaka ushindi mkubwa kuwa na Kocha.

Sawa, tukirudi kwenye somo la leo, Tim anasema wakati anafanya kazi kama Kocha wa Kobe, kazi yake ilikuwa siyo kumsukuma afanye mazoezi, bali kumzuia asifanye mazoezi.
Yaani yeye kama Kocha, kazi yake kubwa ilikuwa kumzuia mchezaji wake asifanye mazoezi.
Hiyo ni kwa sababu Kobe alikuwa anataka kufanya mazoezi muda wote.
Alikuwa anachelewa sana kulala, anawahi sana kuamka na alifanya mazoezi hata siku za mchezo, akifanya mazoezi siku nzima wakati kuna mchezo mkubwa jioni ya siku hiyo hiyo.

Tim anasema Kobe alikuwa na msukumo mkubwa sana ndani yake wa kupata ushindi mkubwa na alikuwa tayari kufanya kila kinachohitajika kufanyika.
Kazi yake haikuwa kumsukuma afanye, bali kumzuia asifanye.
Hiyo ni kwa sababu alitaka mchezaji wake awe na mapumziko ya kutosha ili aweze kufanya maamuzi sahihi na kucheza vizuri wakati wa mashindano makubwa.

Kwenye kitabu chake kinachoitwa Winning, Tim anasema kama inabidi upate msukumo wa nje ndiyo ufanye kitu, kama unasubiri kupewa hamasa ya nje, tayari umeshakosa ushindi mkubwa.
Hebu fikiria tu wewe mwenye, kuna mwenzako ambaye ana msukumo wa ndani wa kupata ushindi, halafu kuna wewe ambaye unasubiri kupata msukumo wa nje, kama mtawekwa kwenye uwanja mmoja, unadhani nani atapata ushindi?

Tukirudi kwa Tim, kuna mambo anaendelea kuyaeleza kwenye kitabu chake ambayo yanaumiza, lakini ndiyo ukweli wenyewe.
Tim anaandika, kama inabidi uambiwe nini ufanye, tayari umeshashindwa kabla hata ya kuanza.
Unapaswa kuwa tayari unajua nini hasa unataka kufanya na Kocha anakusaidia uweze kukifanya kwa ubora.

Hili limenikumbusha maamuzi ambayo nimewahi kuyafanya siku za nyuma na yakanipunguzia sana usumbufu.
Zamani nilikuwa nawapa uzito sana watu wanaosema wanataka kuingia kwenye biashara, ila hawajui ni biashara gani wafanye.
Nilifanya juhudi kubwa ya kuwashauri biashara za kufanya, lakini cha kushangaza ni wachache sana ambao waliingia kwenye biashara kama walivyokuwa wanasema.
Wengi waliendelea kubaki na sababu yao kwamba hawajapata biashara nzuri ya kufanya.

Hapo ndipo niliamua kwamba mtu anayesema anataka kuingia kwenye biashara ila hajui ni biashara gani afanye, nampuuza. Siyo kwa sababu yoyote mbaya, bali kwa sababu anakuwa hajataka kweli kuingia kwenye biashara. Na kama mtu hajataka kitu kweli, hakuna namna unaweza kumbadili kwenye hilo.

Rafiki, kwenye kile unachotaka kupata mafanikio makubwa, je una msukumo wa ndani wa kukifanya muda wote? Au unasubiri kupata msukumo wa nje au msukumo wa mahitaji unayokuwa nayo?
Kwa sababu kama huna ule msukumo wa ndani wa kufaka kufanya muda wote, kama haupo tayari kusahau kula na kuachana na usumbufu mwingine wowote ili ufanye kile ulichochagua, hakuna namna utapata ushindi mkubwa.

Na kwa bahati mbaya sana, hakuna anayeweza kukusaidia upate msukumo mkubwa wa ndani.
Hicho ni kitu unachopaswa kukifanya wewe mwenyewe, kwa kujisikiliza na kuchukua hatua sahihi.

Unachohitaji kutoka kwa wengine siyo msukumo wa kufanya au kuambiwa nini cha kufanya, bali mwongozo wa kufanya kwa usahihi.
Washa moto mkubwa sana ndani yako na utaweza kufanya makubwa ambayo yatawashangaza wengi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe