💯KCM2324052; Kileleni.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#JumatanoYaUwajibikaji

Mwanamafanikio,

Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.

Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.



💯 Neno la leo; Kileleni.

Leo ikiwa ni #JumatanoYaUwajibikaji tunaona jinsi ambavyo siku unayokubali kuwajibika kwako mwenyewe na kuacha kutoa visingizio ndiyo siku unayoanza safari ya kuelekea kileleni.

Kwenye maisha, kuna watu na vitu vimewekwa kwa ajili ya kutufariji pale tunapokuwa tumeshindwa kupata kile tunachotaka.

Namba moja ni wazazi. Kama hujafanikiwa kwenye maisha yako, huwezi kukosa kitu cha kuwalaumu wazazi wako. Utaona wazi kabisa kwamba kuna vitu walifanya au kushindwa kufanya na vimechangia wewe kushindwa kufanikiwa.

Serilali nayo ipo juu kwenye orodha ya kutupiwa lawama pale watu wanaposhindwa.
Halafu kuna vitu kama hali ya hewa, hali ya uchumi na mengine mengi.

Watu wanaweza kutoa lawama kadiri wawezavyo, wanaweza kutoa sababu na visingizio vya kutosha.
Lakini ukweli utabaki kwamba wanaofanikiwa sana siyo watu wa lawama wala visingizio.
Wanaofanikiwa ni watu wa kuwajibika, wa kushika hatamu ya maisha yao wenyewe.

Wanaoyapata mafanikio makubwa ni wale wanaokubali wazi kabisa kwamba chochote kinachotokea kwenye maisha yao ni wao wenyewe wamesababisha.
Wanakuwa wamechagua kuwajibika moja kwa moja na maisha yao.
Na hilo ndiyo linalowafikisha kwenye kilele cha mafanikio makubwa.

Kukwepa uwajibikaji imekuwa breki inayowazuia wengi kufanya makubwa kwa kutumia uwezo mkubwa ambao tayari upo ndani yao.
Ili kuondoa breki hiyo, lazima mtu ukubali kuwajibika moja kwa moja na maisha yako.
Lazima ujue ni wewe unayesababisha kila kitu kwenye maisha yako.
Hapo ulipo sasa ni kwa sababu yako wewe.
Na kule unakotaka kwenda, ni wewe mwenyewe unayewajibika kuhakikisha unafika huko kweli.

Kubali kushika hatamu ya maisha yako, wajibika kwa kila kitu kinachotokea kwenye maisha yako na utaweza kufanya makubwa sana.

💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MJASIRIAMALI MJANJA na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kufanya na kuacha. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/12/20/3276

Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kuanza au kuendelea na safari ya kileleni kwa kuacha kulaumu na kutoa visingizio na kuchagua kuwajibika na maisha yako.

Kocha.
💯