💯KCM2324053; Raha.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#AlhamisiYaUbunifu
Mwanamafanikio,
Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.
Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

💯 Neno la leo; Raha.
Leo ikiwa ni #AlhamisYaUbunifu tunaona jinsi ambavyo ubunifu ni raha ya akili.
Pamoja na kwamba kila mtu ana uwezo wa kuwa na ubunifu mkubwa na wa kipekee, ni watu wachache sana ambao wanadhihirisha ubunifu wao.
Wengi wanayaishi maisha yao bila ya ubunifu wowote, licha ya kuwa na uwezo wa ubunifu ndani yao.
Hilo limekuwa linasababishwa na ugumu na uzito ambao watu wamekuwa wanaweka kwenye ubunifu.
Watu wengi wamekuwa wanachukulia ubunifu kama kitu kikubwa na kigumu, ambacho kinaweza kufanywa na aina fulani tu ya watu.
Hilo siyo kweli, ubunifu siyo kitu kigumu kama wengi wanavyochukulia.
Ubunifu ni zao la akili kuwa na raha.
Pale akili inapokuwa na mzaha, ndiyo ubunifu unapozalishwa.
Ndiyo maana mtu anapojilazimisha kuja na ubunifu fulani ndani ya muda fulani anaokuwa amepanga, huwa hapati ubunifu mzuri.
Lakini akiwa anafanya kitu kingine tofauti kabisa, labda anaoga, anatembea au amepumzika, mawazo ya kibunifu yanawajia.
Bila ya kutumia nguvu wala kujilazimisha, wanapata ubunifu mkubwa.
Hiyo inakuwa ni kwa sababu katika hali hizo akili inakuwa kwenye hali ya raha na hivyo ubunifu kuwa rahisi.
Mara nyingi sana watu wamekuwa wanapata mawazo mazuri na ya kibunifu wakiwa wanafanya kitu cha tofauti na hicho wanachokipatia ubunifu.
Katika hali hizo akili inakuwa haipo kwenye shinikizo la ubinifu, hivyo inakuwa kwenye hali ya raha ambayo inazalisha ubunifu huo.
Watu wengi wamekuwa wanapata mawazo ya kibunifu wanapokuwa wanaoga.
Wakati wa kuoga ndiyo wakati ambao akili ya mtu inakuwa na utulivu mkubwa huku pia ikiwa na raha ya kipekee.
Mazingira hayo yanakuwa mazuri kwa ubunifu kujitokeza.
Kukosa ubunifu ni moja ya breki ambazo zinawazuia wengi kupiga hatua kwenye maisha yao.
Kuachilia breki hiyo ili watu waweze kufanikiwa, akili inapaswa kuwa kwenye hali ya raha na siyo msongo.
Usiilazimishe akili yako kuleta ubinifu, badala yake iachilie iwe huru na kuipa raha na hapo ubunifu utazalishwa wenyewe.
💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MJASIRIAMALI MJANJA na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu hakuna tatizo. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/12/21/3277
Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kuipa akili yako uhuru na raha ili uweze kuwa na ubunifu mzuri na wa kipekee kwenye yale unayofanya.
Kocha.
💯