💯KCM2324054; Macho.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#IjumaaYaMawasiliano

Mwanamafanikio,

Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.

Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.



💯 Neno la leo; Macho.

Leo ikiwa ni #IjumaaYaMawasiliano tunaona jinsi ambavyo macho ni kiungo muhimu kwenye mawasiliano.

Wengi wamezoea kwamba viungo vikuu vya mafanikio ni mdomo na masikio.
Kwamba mmoja anaongea na mwingine anasikiliza.

Ni kweli sehemu kubwa ya mawasiliano inafanyika kwa viungo hivyo viwili.
Lakini ili mawasiliano yakamilike na kuwa na ushawishi, viungo zaidi vinapaswa kuhusika.

Moja ya viungo hivyo ni macho.
Macho ni kiungo muhimu sana kwenye kukamilisha mawasiliano.
Kutumia vizuri macho wakati wa mawasiliano kunayafanya yakamilike kwa uhakika na ushawishi.

Anayeongea anapaswa kumwangalia usoni yule anayesikiliza ili kuona mrejesho wake.
Kwa kutumia macho, anayeongea ataona kama anaeleweka au la.
Kwa kuangalia, ataweza kujua aboresheje kile anachowasilisha ili kuwa na ushawishi zaidi.

Anayesikiliza anapaswa kumwangalia usoni yule anayeongea ili kumwelewa vizuri zaidi.
Kwa kutumia macho, anayesikiliza ataona msisitizo ambao anayeongea anakuwa nao kwenye yale anayowasilisha.
Hilo linamfanya apate uzito sahihi wa kile kinachowasilishwa.

Mawasiliano ya sasa yamekuwa magumu na yasiyobadilika kwa sababu watu wamekuwa hawatumii macho yao wakati wa kuwasiliana.
Macho yao yanakuwa yametekwa na usumbufu mwingine kitu kinachowapunguzia umakini wao na kukwamisha mawasiliano.

Unapowasilisha, hakikisha unawaangalia watu usoni na pia unawafanya wakuangalie. Hilo linafanya umakini wao uwe kwenye kile unachowasilisha.
Unaposikiliza, kazana kuwaangalia watu usoni ili uweze kuelewa vizuri.

Kukosekana au kuvunjika kwa mawasiliano imekuwa ni breki inayowazuia wengi kufanikiwa.
Tumia vizuri macho yako wakati wa mawasiliano ili uweze kuachilia breki hiyo na kufanya makubwa.

💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MJASIRIAMALI MJANJA na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu mafanikio na kupendwa. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/12/22/3278

Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kutumia macho yako vizuri wakati wa mawasiliano ili kuweza kuyakamilisha vizuri.

Kocha.
💯