💯KCM2324056; Mateso.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#JumapiliYaMapumziko
Mwanamafanikio,
Mwaka huu wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kuweka umakini wetu wote kwenye kitu kimoja mpaka kitupe matokeo makubwa.
Na tunaachilia breki kupitia kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kuweza kupiga hatua kubwa.

💯 Neno la leo; Mateso.
Leo ikiwa ni #JumapiliYaMapumziko tunaangalia jinsi ambavyo siku hii inapaswa kuwa ya kupumzisha mateso ya maisha.
Maisha ni mfululizo wa mateso ambayo hayana mwisho mpaka siku unaingia kaburini.
Kila wakati kuna kitu unakuwa unakipambania.
Wengi wasioelewa mwenendo huo wa maisha, hujikuta wakiyaishi maisha yao yote bila ya kuwa na furaha.
Kwa sababu wanakuwa wanakimbizana na kitu kimoja, wakiamini wakishakipata basi watakuwa na furaha milele.
Lakini wanapokipata kile walichokuwa wanakimbiza, wanagundua kuna kikubwa zaidi wanachopaswa kukikimbiza.
Hivyo mbio zinaanza tena upya.
Mfululizo wa maisha ya aina hiyo umegeuka kuwa maisha ya mateso kwa wengi, mateso ambayo hayana mwisho.
Lakini hivyo sivyo maisha yanavyokusudiwa kuwa.
Maisha yanapaswa kuenendwa kwa mtu kupokea kile unachokipata na kukitumia vizuri, huku ukiendelea kupambana na makubwa zaidi.
Kwa kuwa maisha yanaonekana kuwa gurudumu linaloenda bila kusimama na kwa kuwa yale ya kufanya hayana mwisho, mateso ya maisha yamekuwa pia hayana mwisho.
Na hapo ndipo tunapopaswa kuitumia vizuri siku ya jumapili.
Umuhimu wa kuifanya jumapili kuwa siku ya mapumziko, siyo tu kupumzika kufanya kazi, bali pia kupumzisha mateso ya maisha.
Ili kuweza kuitumia siku hii ya jumapili kupumzisha mateso ya maisha, tunapaswa kupotezea yote ambayo huwa yanatusumbua kila kitu.
Tunajipa ruhusa ya kuiishi siku hii moja kama vile tumeshapata kila tunachotaka na maisha yetu yamekamilika kwa kila namna.
Kwenye siku hii tunaachana kabisa na yote yanayotuhangaisha.
Tunaacha kufikiria kazi ambazo bado hatujamaliza.
Tunaacha kufikiria madeni ambayo wengine wanatudai.
Tunaacha kuwafikiria wale wanaotusumbua kwa namna fulani.
Tunachangua kuiishia siku ya jumapili kama watoto wadogo ambao hawana mateso yoyote kwenye maisha.
Hilo linatupa nafasi ya kuwa na mapumziko ya kweli, kimwili, kiakili, kihisia na kiroho.
Maana wengi hutumia siku za jumapili kupumzisha mwili, lakini akili, hisia na roho bado vinakuwa vinaendelea kuteseka.
Tuifanye jumapili kuwa siku ya kusimamisha yote kabisa na tutayafanya maisha yetu kuwa bora hata kama bado hatujapata kila tunachotaka.
💯Hatua za kuchukua leo;
1. Leo ni siku ya mapumziko, wiki nzima umepambana kwa siku 6, siku hii ya 7 tenga muda wa kupumzika ili kukusanya nguvu za kuendelea na mapambano kwenye wiki nyingine.
2. Kamilisha mambo yako binafsi ambayo yalikwama kwa wiki nzima kutokana na kutingwa na shughuli zako za kikazi au kibiashara.
3. Tenga muda wa kupitia wiki unayomaliza na kupangilia wiki inayokwenda kuanza. Angalia yapi umefanya vyema na yapi ya kuboresha. Kisha panga matokeo unayotaka kuzalisha wiki inayofuata.
4. Fanya tathmini yako ya kazi/biashara kwa wiki uliyomaliza. Tathmini hii ihusishe namba muhimu ambazo unajipima nazo kwenye kile unachofanya. Tathmini inakuonyesha hatua ambazo umeshapiga na zile za kuendelea kupiga.
5. Tenga muda wa kutosha kwa watu muhimu kwako ili kujenga na kuimarisha mahusiano yako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kufanya kwa msimamo bila kuacha. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/12/14/3280
Ukawe na siku bora kabisa ya mapumziko leo, siku ya kuyasimamisha mateso ya maisha na kuishi kama umeshapata kila unachotaka.
Kocha.
💯