💯KCM2324058; Ndani.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#JumanneYaKujikubali

Mwanamafanikio,

Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.

Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.



💯 Neno la leo; Ndani.

Leo ikiwa ni #JumanneYaKujikubali tunaona jinsi ambavyo kilicho ndani yako ni kikubwa sana kuliko vyote vya nje.

Watu wengi kwenye maisha huwa wanashindwa kabla hata hawajaanza.
Wanaangalia ukubwa na ugumu wa kile wanachopaswa kufanya na kuona hawataweza kufanya.
Wanaruhusu vitu vya nje viwakwamishe.

Ambacho wanashindwa kuelewa ni kwamba, ndani yao wanao uwezo mkubwa sana wa kuvuka chochote cha nje.
Ukubwa na ugumu wowote unaoonekana kwa nje, hauwezi kufikia uwezo ambao upo ndani ya mtu.

Mtu hawezi kujua ukubwa wa uwezo wake wa ndani mpaka pale anapolazimika kuutumia.
Sasa kwa kuwa watu wanakata tamaa kabla hata ya kujaribu kufanya, wanaona hawawezi au haiwezekani wakati siyo.

Tuangalie mfano rahisi sana ambao wengi tutakuwa na uzoefu nao.
Kunaweza kuwa na ukuta ambao ulikuwa unajiambia huwezi kuuruka au mti ambao uliona huwezi kuukwea.
Lakini siku moja ukawa unakimbizwa na mbwa mkali au kuwa kwenye hatari ya aina hiyo. Kilichotokea ni uliruka ukuta huo au kukwea mti huo bila ya kufikiri mara mbili.

Je unaweza kueleza nini kimekufanya uweze kutekeleza kitu ambacho uliona hakiwezekani kabisa?
Hakuna jibu zaidi ya ndani yako unao uwezo mkubwa sana ambao umekuwa huutumii.

Swali unaloweza kuwa unajiuliza kama kweli uwezo huo upo, kwa nini unashindwa kuutumia kwenye maisha yako ya kila siku? Kwa nini mpaka kuwe na uhitaji mkubwa au hatari ndiyo uweze kutumia uwezo huo?
Na jibu lipo wazi kabisa, ni kwa sababu hujikubali na kujiamini wewe mwenyewe.

Kuweza kufikia na kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yako kunaanza na wewe kujikubali na kujiamini mwenyewe kwanza kabla ya mengine yote.
Ni kupitia kujikubali na kujiamini ndiyo unaweza kukabili kitu chochote, hata kama kinaonekana ni kikubwa kiasi gani.

Kwa chochote kile unachokitaka kwenye maisha yako, anza kwa kujikubali kwamba unaweza kukipata. Jiamini kwamba ndani yako tayari unao uwezo wa kupata hicho unachotaka.
Kisha pambania mpaka ukipate, bila ya kukubali kukwamishwa na chochote kile.

Jikubali kwamba kilicho ndani yako ni kikubwa sana kuliko chochote cha nje kinachokukwamisha.
Anzia hapo na utaweza kuachilia breki zote zinazokuzuia usifanye makubwa.

💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MJASIRIAMALI MJANJA na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kujikwamisha mwenyewe. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/12/26/3282

Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yako kuvuka vikwazo vyote vya nje.

Kocha.
💯