💯KCM2324061; Hadithi.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#IjumaaYaMawasiliano
Mwanamafanikio,
Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.
Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

💯 Neno la leo; Hadithi.
Leo ikiwa ni #IjumaaYaMawasiliano tunaona jinsi ambavyo wanenaji wazuri ni wale ambao wanatumia hadithi kwenye uwasilishaji wao.
Kuwasilisha kitu kwa namna ambayo watu wenye uelewa tofauti wanaweza kupata maana kuu imekuwa ni changamoto kubwa kwa viongozi wengi.
Kiongozi anaweza kuwa na nia njema kabisa kwenye kitu anachofanya. Lakini akakosa kuungwa mkono na wale anaowalenga kwa sababu wameshindwa kumwelewa.
Anaweza kuwa amewaeleza watu vizuri kabisa, kwa mantiki na data sahihi za kitu husika, lakini bado asieleweke.
Hiyo ni kwa sababu uelewa wa watu uko tofauti sana.
Na hata mtazamo ambao watu wanakuwa nao kwenye jambo lolote lile, unatofautiana sana.
Kwenye kitu kimoja, watu wanaweza kuondoka na maana tofauti, kutokana na mtazamo na uelewa wao.
Viongozi na wanenaji wazuri, ambao wamekuwa na ushawishi mkubwa ni wale ambao wamekuwa wanatumia hadithi kwenye uwasilishaji wao.
Faida za kutumia hadithi kwenye mawasiliano na uwasilishaji ni urahisi wake wa kueleweka na wengi lakini pia uwezo wa kubeba taarifa nyingi kwa wakati mmoja.
Ukiangalia viongozi wote mashuhuri na walioweza kuwa na ushawishi mkubwa, ukiangalia walimu na waandishi wote ambao kazi zao zimedumu, wote utaona wakitumia sana hadithi na mifano ambayo ni rahisi kueleweka na wengi.
Kabla ya kuja kwa mfumo rasmi wa elimu, hadithi zilikuwa ndiyo njia kuu ya kufundisha watu mambo yote ya msingi.
Bado mpaka sasa hadithi ni kitu chenye nguvu kubwa ya ushawishi na kueleweka kwa wengi.
Hivyo unapokuwa na taarifa muhimu ya kuwasilisha kwa wengine, tumia hadithi kwenye kuiwasilisha.
Unaweza kutumia hadithi ambazo tayari zipo au hata ukatengeneza hadithi mpya inayoendana na kile unachotaka watu waelewe.
Hadithi zinaeleweka zaidi kwa sababu ya urahisi wake na fursa ya mtu kujiweka kwenye hadithi hiyo.
Mtu anaposikia hadithi huwa anaangalia jinsi ya kujiweka ndani ya hadithi hiyo, kwa kujifananisha na mmoja wa wahusika waliopo kwenye hadithi hiyo.
Mawasiliano yasiyo sahihi yamekuwa breki inayowakwamisha wengi kwenye uwasilishaji na ushawishi.
Kutumia hadithi kwenye uwasilishaji kunaondoa breki hiyo na kuyafanya mawasiliano kukamilika na ushawishi kuwepo.
Tumia hadithi kwenye mawasiliano yako, utafanikisha mengi zaidi kuliko kutokutumia hadithi.
💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MJASIRIAMALI MJANJA na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu siyo kwa ajili yako. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/12/29/3285
Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kutumia hadithi kwenye mawasiliano ili kufikisha ujumbe vizuri na kuwa na ushawishi mkubwa.
Kocha.
💯