💯KCM2324062; Kujikumbuka.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#JumamosiYaUtulivu
Mwanamafanikio,
Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.
Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.
💯 Neno la leo; Kujikumbuka.
Leo ikiwa ni #JumamosiYaUtulivu tunaona jinsi ambavyo mtu unajikumbuka kwenye utulivu.
Kwenye hii dunia inayokwenda kasi sana, huku mambo ya kufanya yakiwa mengi na muda ukiwa mchache, kupata muda binafsi wa kuwa na utulivu kimekuwa kitu kigumu sana.
Kadiri mtu anavyohangaika na mambo mengi na kukosa muda kwa ajili yake ndivyo anavyojisahau yeye mwenyewe.
Na mtu anavyokwenda hivyo kwa muda mrefu, anakuja kuwa kama mgeni kwake yeye mwenyewe.
Hilo ndiyo limekuwa linapelekea watu kushindwa kuyafurahia matokeo wanayoyapata.
Kwa sababu wakati wanayapambania, wanakuwa wamejisahau kabisa wao wenyewe.
Haijalishi maisha yanakwenda kasi kiasi gani, unapaswa kutenga muda wa utulivu kwako binafsi.
Hiyo siyo anasa wala kupoteza muda, bali ni kuhakikisha muda unaoweka kwenye yale unayofanya unakuwa sahihi na wenye tija.
Hekima inaishi kwenye utulivu.
Amani inapatikana kwenye utulivu.
Utajikumbuka ukiwa kwenye utulivu.
Ili yote unayohangaika nayo yawe na tija, ni lazima yaambatane na utulivu.
Kukosa utulivu imekuwa breki inayowazuia wengi wasipige hatua kubwa kwenye maisha yao.
Kwa kuona utulivu kama anasa na upotevu wa muda, wanahangaika na mengi yasiyokuwa na tija.
Hiyo ni kwa sababu wanakuwa wamekosa hekima na amani, kitu kinachopelekea wajisahau wao wenyewe.
Achilia breki hiyo kwa kutenga muda wa utulivu, muda wa wewe kuwa na wewe mwenyewe.
Wewe unajijua zaidi, unapokaa na wewe mwenyewe, unajikumbusha yale muhimu kukuhusu na kuyazingatia kwenye yale unayoyapambania.
💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MJASIRIAMALI MJANJA na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kushangazwa na dunia. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/12/30/3286
Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kutumia utulivu kujijengea hekima, kupata amani na kujikumbuka wewe mwenyewe.
Kocha.
💯