💯KCM2324063; Asili.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#JumapiliYaMapumziko
Mwanamafanikio,
Mwaka huu wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kuweka umakini wetu wote kwenye kitu kimoja mpaka kitupe matokeo makubwa.
Na tunaachilia breki kupitia kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kuweza kupiga hatua kubwa.

💯 Neno la leo; Asili.
Leo ikiwa ni #JumapiliYaMapumziko tunaangalia jinsi ambavyo siku hii inapaswa kuwa ya kuungana na asili ambayo ulitengana nayo kwa juma zima.
Kuna mabadiliko mengi sana ambayo maisha ya kisasa yameleta.
Kwa namna tunavyoishi kila siku na shughuli tunazofanya, tumetengana sana na asili.
Kutokana na kutingwa na kazi, mtu anaweza kwenda wiki nzima hajakanyaga ardhi.
Wengi hawapati hata kuwakiwa na jua kiasi cha kutosha.
Kwa kifupi, maisha ya sasa yametutenga sana na asili.
Huko kutengana na asili kumekuwa ndiyo chanzo cha changamoto nyingi ambazo watu wanakutana nazo.
Kuanzia kwenye maradhi mbalimbali ambayo watu wanayapata, mpaka kwenye uchoshi na msongo.
Vyote hivyo vinachochewa sana na kutengana na asili.
Hivyo moja ya mambo ya kufanya na ambayo yatakuwa na msaada ni kutenga siku ya kurejea kwenye asili.
Kwa kuwa siku nyingine za wiki watu wanakuwa wametingwa sana, siku ya jumapili ambayo wengi wana mapumziko ndiyo nzuri kufanya hivyo.
Itenge kila jumapili yako kuwa siku ya kurejea kwenye asili ili kuweza kurekebisha matatizo na changamoto mbalimbali zinazokuwa zinajijenga kwa mtu.
Jumapili kanyaga ardhi, kaa juani, tembea porini, tembea ufukweni, fanya tahajudi na kutana na watu mbalimbali.
Mengi utakayofanya na kukamilisha yatapunguza sana matatizo na changamoto ambazo zinajitengeneza ndani yako.
Itenge kila jumapili kama siku yako ya kurejea kwenye asili ili uweze kupata mapumziko na kutatua mambo mengine ya ndani yako.
💯Hatua za kuchukua leo;
1. Leo ni siku ya mapumziko, wiki nzima umepambana kwa siku 6, siku hii ya 7 tenga muda wa kupumzika ili kukusanya nguvu za kuendelea na mapambano kwenye wiki nyingine.
2. Kamilisha mambo yako binafsi ambayo yalikwama kwa wiki nzima kutokana na kutingwa na shughuli zako za kikazi au kibiashara.
3. Tenga muda wa kupitia wiki unayomaliza na kupangilia wiki inayokwenda kuanza. Angalia yapi umefanya vyema na yapi ya kuboresha. Kisha panga matokeo unayotaka kuzalisha wiki inayofuata.
4. Fanya tathmini yako ya kazi/biashara kwa wiki uliyomaliza. Tathmini hii ihusishe namba muhimu ambazo unajipima nazo kwenye kile unachofanya. Tathmini inakuonyesha hatua ambazo umeshapiga na zile za kuendelea kupiga.
5. Tenga muda wa kutosha kwa watu muhimu kwako ili kujenga na kuimarisha mahusiano yako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu watu kubadilila. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/12/31/3287
Ukawe na siku bora kabisa ya mapumziko leo, siku ya kurudi kwenye asili ili kutatua matatizo na changamoto mbalimbali zinazojengeka ndani yako.
Kocha.
💯