Kwenye safari ya mafanikio, watu huwa wanajaribu vitu mbalimbali ili kuweza kupata matokeo ambayo wanayataka.
Mwanzoni siyo vibaya kujaribu vitu vingi, kwa sababu mtu unakuwa unajitafuta. Lakini kama mtu ataendelea kufanya vitu mbalimbali kwa muda mrefu, hataweza kupata mafanikio makubwa anayoyataka.
Baada ya kujaribu baadhi ya vitu na mtu kuona kile ambacho kina uwezo wa kukupa matokeo unayoyataka, unapaswa kuacha kujaribu vitu vipya kila wakati na kutumia kanuni ya Wingi, Ubora, Upya kupata matokeo unayoyataka.

Hatua ya kwanza ni WINGI; Hapa unafanya kwa wingi kile ambacho kimeonyesha kukupa matokeo unayoyataka. Unafanya kwa wingi sana kwa sababu ni kupitia wingi ndiyo unaweza kupata matokeo unayoyataka. Kwa kufanya kwa wingi utaweza kupata matokeo halisi kama kitu kinaweza kuleta matokeo makubwa au la.
Swali unaloweza kujiuliza ni kwa wingi kiasi gani unapaswa kufanya. Na namba ya chini ya kuanzia ni MARA 10 ya kiasi cha juu kabisa cha ufanyaji unachoweza kufanya. Ndiyo, kile kiasi cha juu unachoona unaweza kufanya, zidisha mara 10 na hilo ndiyo linapaswa kuwa lengo la kufikia kufanya kabla hujasema kitu hakileti matokeo.
Baada ya kufanya kwa wingi mpaka kumaliza kabisa uwezo uliopo, ndipo sasa unaenda kwenye UBORA. Hapa unaangalia namna ya kuboresha kile ambacho umeshafanya kwa wingi ili kuzalisha matokeo makubwa zaidi ya yale ambayo tayari yanapatikana. Kwenye hatua hii unaangalia ni namna gani bora zaidi ya kufanya kile kinachofanyika ili matokeo yaweze kuwa makubwa zaidi.
Ni muhimu sana ubora uje baada ya wingi, kwa sababu kupitia wingi ndiyo utajua kama kitu kinafanya kazi. Ukishakuwa na uhakika kinafanya kazi, hapo unaweza kuboresha ili kifanye kazi vizuri zaidi.
Kufanya kwa UPYA kunakuja baada ya wingi na ubora kufika mwisho. Hapo ndipo mtu unapaswa kuangalia kipi kipya cha kufanya ili kupata matokeo ambayo ni makubwa zaidi. Kwa kufanya kitu kipya, unagusa maeneo ambayo hukuwa unayagusa kupitia ufanyaji wa awali.
Mfululizo unapaswa kwenda hivyo, anza kwa wingi, kisha ubora halafu ndiyo upya. Hivyo ndivyo unavyoweza kuzalisha matokeo makubwa na ya uhakika.
Kwa bahati mbaya sana, watu wamekuwa wanaenda kinyume, wamekuwa wanakimbizana na vitu vipya kila wakati na hawapati matokeo wanayotaka. Hiyo ni kwa sababu matokeo hayatokani na upya, bali wingi na ubora. Baada ya kujaribu vitu vipya, lazima uchague kimoja ambacho utakifanya kwa kina zaidi. Hicho ndiyo utakifanya kwa ukubwa sana, kisha kwenda kwa ubora kabla hujaenda kwenye kingine kipya.
Kanuni hii inafanya kazi kwenye kila eneo la maisha. Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeizungumzia kwa upande wa mauzo ili mtu uweze kuifanyia kazi na kukuza mauzo yako.
Sikiliza kipindi hicho hapo chini ili uweze kujifunza na kuchukua hatua ili uweze kuboresha maisha yako na kukuza zaidi mauzo yako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 2. KISIMA CHA MAARIFA, 3. CHUO CHA MAUZO na 4. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.