💯KCM2324067; Unganisha.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#AlhamisiYaUbunifu

Mwanamafanikio,

Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.

Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

Ndani yako una nguvu kubwa sana, hebu itumie vizuri ili kufanya makubwa. 0678 977 007 kupata kitabu.



💯 Neno la leo; Unganisha.

Leo ikiwa ni #AlhamisiYaUbunifu tunaona jinsi ambavyo ubunifu ni kuunganisha vitu.

Ubunifu unaonekana kama kitu kigumu sana kwa walio wengi, kwa sababu wanauwekea uzito mkubwa sana.

Uzito huo ambao watu wanauweka kwenye ubunifu unafunga akili zao zisiweze kuwaletea ubunifu ambao ungeweza kuboresha yale wanayofanya.

Kimsingi ubunifu huwa ni kuunganisha vitu ambavyo kwa kawaida havina muunganiko.
Hivyo ili uweze kufanikisha hilo ni lazima mtu uwe na udadisi na utayari wa kujaribu vitu ambavyo pia unaweza kukosea.

Unapoangalia vitu, hata kama havina uhusiano wa karibu, unapaswa kujiuliza kama vingeungana pamoja, nini kingetokea?

Kwa kuanza na swali la aina hiyo na kujaribu baadhi ya vitu inakuletea matokeo ya tofauti ambayo ndiyo ubunifu wenyewe.

Ubunifu siyo kuja na kitu kipya kabisa ambacho hakijawahi kuwepo, bali ni kuunganisha kwa utofauti vitu ambavyo tayari vipo.

Hata ukiangalia maendeleo makubwa ambayo yametokea duniani, hayajatokana na vitu vipya ambavyo havikuwepo, bali matumizi ya tofauti ya vitu ambavyo tayari vilikuwepo.

Umeme jua ni kitu kilichogunduliwa miaka siyo mingi sana. Lakini jua limekuwepo tangu enzi na enzi. Kwa nini miama mingi ya nyuma hawakuweza kutumia jua kuzalisha umeme?
Ni kwa sababu kuna vitu walishindwa kuunganisha.

Injini ya kwanza na ambayo ndiyo ilileta mapinduzi ya viwanda ilikuwa ni ya mvuke wa maji. Mvuke siyo kitu kipya, kimekuwepo wakati wote. Lakini watu hawakuwa wameweza kuunganisha mvuke na mwendo ili kupata injini.

Angalia kila aina ya ubunifu unaouona, kisha nenda nyuma yake, utajionea dhahiri kwamba hakuna kipya kabisa. Utaona wazi kwamba ubunifu ni muunganiko wa tofauti wa vitu ambavyo tayari vipo.

Kuna vitu vingi ambavyo tayari vipo mbele yako kila siku, viunganishe pamoja ili uweze kuzalisha matokeo ya tofauti na yenye tija zaidi.

Kuwa na ubunifu ni moja ya njia za kuachilia breki zinazowakwamisha wengi kupiga hatua kubwa, hasa kwenye kuja na vitu vya tofauti.
Usijiambie tena kwamba wewe siyo mbunifu.
Tayari unao ubunifu mkubwa ndani yako, unachokosa ni udadisi na kujaribu kuunganisha vitu pamoja.

Tumia ubunifu ambao tayari upo ndani yako, kwa kuunganisha vitu pamoja ili uweze kuleta matokeo ya tofauti.
Usiogope kujaribu vitu vipya na vya tofauti, hata kama matokeo hayatakuwa kama ulivyotaka, bado kuna mengi ambayo utajifunza na yatakufungua zaidi.

💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MWONGOZO WA MAISHA YA MAFANIKIO na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kupambania unachotaka. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2024/01/04/3291

Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kuunganisha vitu vilivyopo ili kuweza kupata ubunifu ubunifu mpya na utakaokupa matokeo makubwa.

Kocha.
💯