Maisha ni mfululizo wa changamoto zisizokuwa na ukomo. Unapotatua changamoto moja, unakuwa umetengeneza changamoto nyingine. Hivyo ndivyo maisha yetu hapa duniani yanavyokwenda mpaka siku tunayokufa.
Watu wasiojua ukweli huu kuhusu maisha, wamekuwa wakiteseka kwa maisha yao yote. Kila wanapokuwa na changamoto na kukazana kuitatua, wanakuwa na matumaini kwamba wakishamaliza kuitatua basi wamemaliza kila kitu. Ni pale wanapomaliza kutatua changamoto hiyo moja na kukutana na nyingine ikiwa inawasubiri ndiyo wanaona maisha yao ni magumu.

Zipo falsafa, dini na imani mbalimbali ambazo watu wanazitumia kama nguzo ya kukabiliana na mambo mbalimbali kwenye maisha yao. Baadhi ya falsafa, dini na hata imani hizo zimekuwa zinawaongezea watu changamoto zaidi kuliko kuzitatua. Yaani zinawageuza watu kuwa watumwa na maisha yao kuwa ya hovyo zaidi.
Lakini kuna falsafa moja ambayo ni mahususi kwa ajili ya kuwawezesha watu kuyavuka magumu na changamoto za maisha na kuwaacha wakiwa imara. Kwa kuishi falsafa hiyo, mtu anavuka changamoto akiwa bora zaidi kuliko alivyokuwa kabla ya changamoto hiyo. Lakini pia anakuwa tayari kukaribisha changamoto nyingine yoyote bila ya hofu.
Hiyo ni falsafa ya USTOA, falsafa iliyoanzia Ugiriki ya kale kisha kuhamia Roma ya kale. Falsafa hii imeweza kusalia kwa miaka mingi sasa kwa manufaa yake makubwa ambayo imekuwa inawapa wale wanaoiishi.
Imekuwa ni falsafa ambayo viongozi, wanajeshi, wajasiriamali, wachezaji na watu wengine ambao kazi zao zinawapa msongo mkubwa, wanaitumia kupata utulivu. Falsafa hii inampa mtu uimara wa kukabiliana na chochote bila ya hofu wala kukata tamaa.
Habari njema ni kwamba na wewe pia unaweza kuiishi falsafa hii na ukawa imara kwenye kukabiliana na kila aina ya changamoto za maisha.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA, nimeeleza misingi 10 muhimu ya falsafa ya Ustoa ambayo unapaswa kuijua na kuiishi ili uweze kuwa na maisha bora na kukabili kila aina ya changamoto. Karibu usikilize kipindi hicho hapo chini na uanze kuiishi misingi ya Ustoa ili kuwa na maisha imara.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 2. KISIMA CHA MAARIFA, 3. CHUO CHA MAUZO na 4. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.