💯KCM2324070; Ushindi.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#JumapiliYaMapumziko

Mwanamafanikio,

Mwaka huu wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kuweka umakini wetu wote kwenye kitu kimoja mpaka kitupe matokeo makubwa.

Na tunaachilia breki kupitia kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kuweza kupiga hatua kubwa.

0678 977 007 kupata vitabu.



💯 Neno la leo; Asili.

Leo ikiwa ni #JumapiliYaMapumziko tunaangalia jinsi ambavyo siku hii ni ya kupanga ushindi wa wiki inayofuata.

Jumapili ni siku ya mwisho kwenye wiki, siku ambayo ni ya mapumziko.
Mapumziko haya ya jumapili siyo ya kustarehe na kujihangaisha na mambo yasiyokuwa na tija.
Bali ni siku ya kupitia jinsi wiki nzima ilivyokwenda na kupanga ushindi mkubwa zaidi kwenye wiki inayofuata.

Kitendo tu cha kufika siku ya jumapili ni ushindi mkubwa. Kwani hata kama hujapata matokeo iliyotaka kupata, kuna mengi ambayo umejifunza.
Unapotenga siku hiyo ya jumapili na kuyapitia yote uliyojifunza, ni ushindi mkubwa.
Na ushindi mkubwa zaidi ni pale unapotumia hayo uliyojifunza kupangilia wiki inayofuata ili kwenda kufanya kwa ubora zaidi.

Watu wengi wamekuwa wanayapoteza maisha yao kwa kujiendea tu kwa mazoea.
Kila siku wanarudia kufanya yale waliyozoea kufanya.
Wanaendelea kupata matokeo yale yale ambayo wamekuwa wanayapata.
Na bado wanaendelea na mazoea.

Wengi huona kutenga siku ya kutafakari na kupitia siku nyingine walizoweka kazi ni kupoteza.
Lakini kiuhalisia wanakuwa wanapoteza zaidi kwa kwenda kwa mazoea kuliko muda wanaoona wanauongeza kwa kutokupumzika.

Ifanye jumapili kuwa siku bora kabisa kwako kwenye wiki yako nzima.
Itumie kupitia siku zote za wiki na kupima ushindi ambao umeupata.
Kisha panga ushindi mkubwa zaidi kwa wiki inayokuwa inafuata.
Ukiweza kwenda hivyo kwa msimamo bila kuacha, utaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yako.

Kupumzika, kutafakari na kutathmini siyo kupoteza muda, bali ni kujikusanya ili kufanya kwa ukubwa na ubora zaidi.
Tumia siku ya jumapili kwa hayo ili uweze kufanya makubwa zaidi kwenye maisha yako.

💯Hatua za kuchukua leo;
1. Leo ni siku ya mapumziko, wiki nzima umepambana kwa siku 6, siku hii ya 7 tenga muda wa kupumzika ili kukusanya nguvu za kuendelea na mapambano kwenye wiki nyingine.
2. Kamilisha mambo yako binafsi ambayo yalikwama kwa wiki nzima kutokana na kutingwa na shughuli zako za kikazi au kibiashara.
3. Tenga muda wa kupitia wiki unayomaliza na kupangilia wiki inayokwenda kuanza. Angalia yapi umefanya vyema na yapi ya kuboresha. Kisha panga matokeo unayotaka kuzalisha wiki inayofuata.
4. Fanya tathmini yako ya kazi/biashara kwa wiki uliyomaliza. Tathmini hii ihusishe namba muhimu ambazo unajipima nazo kwenye kile unachofanya. Tathmini inakuonyesha hatua ambazo umeshapiga na zile za kuendelea kupiga.
5. Tenga muda wa kutosha kwa watu muhimu kwako ili kujenga na kuimarisha mahusiano yako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kuonekana, kuweka kazi na kusikiliza. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2024/01/07/3294

Ukawe na siku bora kabisa ya mapumziko leo, ya kutathmini wiki nzima ilivyokwenda na kupanga ushindi mkubwa zaidi kwa wiki inayofuata.

Kocha.
💯