KCM2324071; Shikilia.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#JumatatuYaMalengo

Mwanamafanikio,

Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.

Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

 Neno la leo; Shikilia.

Leo ikiwa ni #JumatatuYaMalengo tunaona jinsi ambavyo kushikilia uwezo wako mkubwa kwenye eneo moja ndiko kunakozalisha matokeo makubwa.

Kuna watu wenye akili nyingi sana ila hawana matokeo makubwa. Wakati kuna watu wenye akili za kawaida ila wana matokeo makubwa.

Kuna watu wana vipaji vikubwa ila hakuna cha tofauti wamefanya. Wakati kuna wenye vipaji vya kawaida na wameweza kufanya ya tofauti.

Kuna watu wana kipato kikubwa ila hawajaweza kujenga utajiri. Wakati kuna wenye kipato cha kawaida na wameweza kujenga utajiri mkubwa.

Tunachoona hapo, na ndivyo ilivyo kwenye maisha, kuna tofauti kubwa kati ya uwezo na matokeo.
Mara nyingi uwezo unapokuwa mkubwa, matokeo huwa hayaendani na uwezo huo.

Hiyo ni kwa sababu wenye uwezo huo mkubwa huwa wanaridhika na kudhani uwezo pekee unatosha.
Na ndiyo maana utakuta hao hao wenye uwezo mkubwa ndiyo wanaongoza kwa kuanzisha mambo mengi na kuishia njiani.

Matokeo yoyote makubwa yanazalishwa kwa kufanyia kitu kazi kwa muda mrefu.
Bila ya kujali uwezo wa mtu, muda unahitajika kwenye kujenga chochote kikubwa.
Hilo linataka uvumilivu mkubwa, ambao watu wenye uwezo mkubwa huwa hawana.
Huwa wanadhani kwa uwezo wao mkubwa hawastahili kusubiri kama wengine.

Haijalishi una uwezo mkubwa kiasi gani, kupata matokeo makubwa, lazima ulenge uwezo huo kwenye uelekeo mmoja na kushikilia hapo kwa muda mrefu.
Ni mkusanyiko wa uwezo huo kwenye eneo moja na kwa muda mrefu ndiko kunakuwa na nguvu ya kuleta matokeo makubwa sana.

Hilo linajidhihirisha hata kwenye asili.
Mwanga wa jua umetawanyika na unamulika.
Mwanga huo ukikusanywa kwenye eneo moja kwa kutumia lensi, unaweza kuunguza kabisa.
Lakini mkusanyiko huo wa mwanga utaunguza kama utashikiliwa mahali pamoja kwa muda.
Pamoja na mwanga kukusanywa, kama utaendelea kuhamishwa hamishwa, hautaweza kuzalisha moto unaoweza kupatikana.

Zijue rasilimali zote muhimu zilizo ndani yako, kisha zielekeze kwenye kile unachotaka na zishikilie hapo kwa muda mrefu zaidi bila kuyumba.
Itakuwa swala la muda tu kupata kile unachotaka.

Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MWONGOZO WA MAISHA YA MAFANIKIO na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu ufuatiliaji wa karibu. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2024/01/08/3295

Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kulenga na kushikilia rasilimali zako zote kwenye kile unachotaka bila kuyumba mpaka ukipate.

Kocha.