Ili kujenga utajiri na uhuru wa kifedha, unapaswa kuwa na vyanzo vingi vya kipato. Kama ni biashara, uwe nazo zaidi ya moja. Hili ni jambo muhimu sana, lakini limekuwa linawapotosha wafanyabiashara wengi.

Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanakimbilia kuwa na biashara nyingi mapema kabla hawajafikia hatua sahihi ya kufanya hivyo. Kuanza biashara zaidi ya moja kwa wakati mmoja ni njia ya uhakika ya kushindwa kwenye biashara.

Lakini pia kuwa na biashara zaidi ya moja na zote zinategemea uwepo wako ili kuweza kwenda, nako pia unajikwamisha kufanikiwa. Unahitaji kufika hatua ya biashara kutokukutegemea kwenye uendeshaji wake ndiyo uweze kuanzisha biashara nyingine.

Biashara ni kama kiumbe hai, kwenye hatua zake za awali kinakuwa na utegemezi mkubwa kwa mzazi. Mtoto mchanga anamtegemea mama yake kumnyonyesha ndiyo aweze kupata afya nzuri. Pale mzazi anaposhindwa kumnyonyesha mtoto vizuri ndiyo wanasema mtoto amebemendwa.

Kadhalika kwenye biashara, pale mtu anapoanzisha biashara ya pili, wakati ya kwanza bado inamtegemea anakuwa anaibemenda hiyo ya kwanza. Matokeo yake ni biashara zote mbili zinadumaa na hata kufa.

Pamoja na malengo makubwa uliyonayo ya kuwa na biashara zaidi ya moja, unapaswa kuanza na biashara moja kwanza, kuiendesha vizuri mpaka pale itakapoweza kujiendesha bila ya kukutegemea moja kwa moja kisha kwenda kuanzisha biashara nyingine. Hiyo ndiyo hatua muhimu unayopaswa kuifikia kibiashara ndiyo uweze kuwa na biashara zaidi ya moja.

Swali maarufu kwa wengi ni vipi kama mtu umeshakuwa na biashara zaidi ya moja na zote zinakutegemea wewe moja kwa moja. Na hapo jibu ni la wazi kabisa, chagua biashara moja ambayo unaona ukiiwekea nguvu zako zote itakupa matokeo unayoyataka. Kisha funga biashara nyingine zote na weka nguvu zako kwenye biashara hiyo moja.

Baadaye ukishaifikisha biashara hiyo moja kwenye hatua ya kutokukutegemea, utaweza kufanya biashara nyingine kadiri utakavyo. Kama utajiambia biashara zote zinakulipa vizuri, jua hujawa tayari kupata ukuaji mkubwa kuliko malipo unayotaka. Kama biashara mbili zinazokutegemea zinakulipa vizuri, ukipeleka nguvu hizo kwenye biashara moja, itakulipa kwa ubora zaidi.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA, nimeeleza kwa kina mambo kumi ya msingi ya kuzingatia kwenye kujenga biashara inayoweza kujiendesha yenyewe bila kukutegemea kabla ya kuwa na biashara zaidi ya moja.

Karibu usikilize kipindi hicho hapa chini.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 2. KISIMA CHA MAARIFA, 3. CHUO CHA MAUZO na 4. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.