Biashara ni kama kiumbe hai, ambacho uhai na ukuaji wake unategemea uwepo wa viungo vya msingi.

Kwetu binadamu, mtu anakuwa hai pale anapokuwa anapumua na mapigo ya moyo yapo. Pumzi zinatupa hewa na mapigo ya moyo yanasukuma damu, hewa na damu ni vitu viwili muhimu kwa uhai wa mwanadamu.

Kwenye biashara, hewa ni wateja na damu ni fedha, biashara ikikosa vitu hivyo viwili, yaani wateja na fedha, lazima itakufa. Wateja wanapatikana kwa pumzi ya masoko na fedha zinapatikana kwa mapigo ya moyo ambayo ni mauzo.

Kwa maana hiyo basi, mauzo ndiyo moyo wa biashara, bila mauzo hakuna biashara. Kutokana na umuhimu huo mkubwa wa mauzo, kila mtu aliyepo kwenye biashara anapaswa kuyafanya mauzo kuwa kipaumbele chake namba moja.

Lakini ni jambo la kusikitisha sana kwamba wafanyabiashara wengi wanayachukulia mauzo kawaida tu. Wanakuwa hawana malengo wala mkakati wowote wa kukuza zaidi mauzo. Kwa ambao mauzo yanakua, inakuwa imetokana na sababu za nje na siyo za ndani, mfano msimu kuwa mzuri. Kwa kutegemea sababu za nje, ukuaji wa mauzo umekuwa siyo wa kudumu.

Ndiyo maana mauzo ya wafanyabiashara wengi yamekuwa ya kupanda na kushuka. Kuna wakati wanauza sana, pale mambo yanapokuwa mazuri na mambo yakiwa mabaya mauzo yanashuka sana.

Ipo njia ya kuweka malengo na mikakati ambayo itaiwezesha biashara kukuza mauzo yake mara mbili na zaidi ndani ya mwaka mmoja. Kwa kufanya hivyo, ile hali ya kupanda na kushuka sana kwa mauzo inaondoka. Hata kama mauzo hayatalingana mara zote, lakini yatakuwa juu kuliko ilivyo kwa wasio na mkakati kama wako.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza kwa kina mkakati huo wa kuweza kukuza mauzo mara mbili kwenye biashara yako. Sikiliza kipindi hicho hapo chini na uondoke na mambo ya kwenda kufanyia kazi ili kukuza mauzo ya biashara yako.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 2. KISIMA CHA MAARIFA, 3. CHUO CHA MAUZO na 4. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.