Habari Matajiri Wawekezaji,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo ya programu maalumu ya NGUVU YA BUKU.
Hii ni programu ya kujifunza na kujenga utajiri kwa uhakika kwa kuanzia popote pale ambapo mtu yupo.

Mtu yeyote mzima, mwenye afya na akili timamu, anao uwezo wa kujenga utajiri kwenye maisha yake kama atazichanga karata zake vizuri.

Kuna karata kuu tatu ambazo kila mtu anapaswa kuzichanga vizuri ili kujijengea utajiri.
Karata hizo ni KIPATO, UWEKEZAJI na MUDA.
Karibu ujifunze jinsi ya kuzichanga karata hizi vizuri na tusafiri pamoja kwenye kujenga utajiri.

Karata ya Kipato.

Kipato ambacho mtu anaingiza ndiyo mbegu kuu ya kujenga utajiri kwenye maisha yake.
Wengi huwa wanadharau vipato vidogo vidogo wanavyoingiza na kusubiri mpaka wawe na kipato kikubwa ndiyo wajenge utajiri.

Lakini kama ulivyo usemi maarufu, madogo yakikushinda, makubwa hutayaweza.
Kama utashindwa kuanza kujenga utajiri kwa kipato kidogo, basi jua hata kikubwa kitakushinda.
Kama unashindwa kuweka akiba kwenye kipato kidogo, usidhani kuna miujiza itakayotokea kipato kikiwa kikubwa.

Kwenye kipato, unapaswa kuwa na vyanzo vingi vya kuingiza kipato ili usikwame pale chanzo kimoja kinapopata changamoto.
Kama umeajiriwa, hakikisha pia unakuwa na biashara yako ya pembeni, unayoweza kuifanya kwenye muda wako wa ziada na ikakuingizia kipato.
Kwenye biashara hakikisha unakuwa na wateja wengi na ambao wanathamini kile unachouza.
Hao ndiyo utakaoweza kuwahudumia kwa uhakika na kuingiza kipato kikubwa.

Kila mara hakikisha unakuza zaidi kipato chako kwa kutoa thamani kubwa zaidi.
Kipato unachoingiza sasa ni matokeo ya thamani unayotoa.
Ukitaka kuingiza kipato zaidi, toa thamani kubwa zaidi.

Karata ya Uwekezaji.

Uwekezaji ni kuifanya fedha yako ikufanyie kazi na kukuingizia faida bila ya wewe kufanya kazi moja kwa moja.

Ukiwa na nguvu za kufanya kazi na kuingiza kipato moja kwa moja unaweza kubweteka na kudhani maisha yako yataenda hivyo.

Lakini umri unavyokwenda, nguvu zinapungua na unakuwa huwezi tena kuweka juhudi kubwa.
Lakini mahitaji ya maisha bado yanakuwepo.
Hapo ndipo unapohitaji kuwa na vyanzo vinavyokuingizia kipato bila kufanya kazi moja kwa moja.

Uwekezaji ni kitu kinachopaswa kuanza mapema.
Yaani ingepaswa pale tu mtu anapopokea kipato chake cha kwanza kwenye maisha, tangu akiwa mtoto basi aanze kuwekeza.

Lakini kwa sababu wengi hawana elimu ya uwekezaji na wala kwenye jamii nyingi hakuna watu wa mfano kwenye uwekezaji, wengi wamekuwa hawawekezi kabisa.

Lakini pia kuna uwekezaji ambao watu wanafanya, lakini hauwi na manufaa kwao. Mfano mtu anapowekeza kwenye ujenzi wa nyumba ya kuishi.
Ni kitu kizuri kufanya, lakini kukiita uwekezaji siyo sahihi.
Kwa sababu hata kama nyumba hiyo itapanda thamani, bado haitaweza kuzalisha kipato bila mtu kufanya kazi.

Hivyo unapofanya uwekezaji wowote, hakikisha baadaye kuna njia ya wewe kuingiza kipato bila ya kufanya kazi moja kwa moja.

Kwenye uwekezaji, kanuni muhimu ni anza mapema na wekeza kwa muda mrefu, kwa msimamo bila kuacha.

Karata ya Muda.

Muda ni kiungo muhimu sana kwenye kujenga utajiri.
Muda utakwenda, iwe unachukua hatua au la.
Iwe unaongeza kipato au la, muda unakwenda.
Iwe unawekeza au huwekezi, muda unakwenda.
Kwa kifupi, muda haumsubiri mtu yeyote, unaendelea kwenda.

Kuutumia muda kwenye kujenga utajiri, zingatia mambo mawili muhimu.

Moja ni kuhakikisha kadiri muda unavyokwenda, kipato chako kinakuwa kinaongezeka.
Usikubali mwaka uanze na kuisha huku wewe ukiwa na kipato kile kile.
Tumia muda wako vizuri kujifunza na kubobea kwenye kile unachofanya ili uweze kutoa thamani kubwa zaidi na kuongeza kipato chako.

Mbili ni tumia nguvu ya muda kwenye kuwekeza. Pale unapofanya uwekezaji kwa muda mrefu bila kuuingilia, ndivyo unavyonufaika zaidi na riba mkusanyiko.
Hapo riba unayokuwa unapata kwenye uwekezaji wako na yenyewe pia inazaa riba.
Hivyo muda unavyokwenda, unakuta umezalisha faida kubwa kuliko kiasi ulichowekeza.
Hivyo kunufaika na muda kwenye uwekezaji, anza mapema na wekeza kwa muda mrefu bila kuacha au kuingilia uwekezaji wako.

Hizi ndizo karata tatu za kuchanga vizuri ili ujenge utajiri kwenye maisha yako.

Mjadala wa somo hili;
Kwenye maoni hapo chini, shirikisha yafuatayo;

  1. Una mkakati gani kwenye kuongeza zaidi kipato chako?
  2. Umekuwa unawekeza kwa miaka mingapi sasa? Uwekezaji unaofanya sasa, unapanga kwenda nao kwa miaka mingapi?
  3. Unahakikishaje unautumia muda kwa manufaa kwenye kuongeza kipato na kukuza uwekezaji?

Shirikisha majibu ya maswali hayo kama sehemu ya kujifunza na kuelewa somo hili.

Kutoka kwa tajiri mwekezaji mwenzako,
Kocha Dr Makirita Amani
http://www.utajiri.tz/kitabu