KCM2324075; Chakusema.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#IjumaaYaMawasiliano

Mwanamafanikio,

Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.

Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

 Neno la leo; Chakusema.

Leo ikiwa ni #IjumaaYaMawasiliano tunaona jinsi ambavyo mawasiliano yalivyo tofauti kwa wapumbavu na werevu.

Wapumbavu huwa wanaongea kwa sababu wana kitu cha kusema.
Wanaona imefika zamu yao ya kuongea na hivyo wanapaswa kuongea.
Kwa njia hiyo, hujikuta wanaongea mambo hata yasiyokuwa na tija, ili tu waonekane na wao wameongea.

Werevu huwa wanaongea kwa sababu wana kitu cha kuchangia. Wanaona wana mchango kwenye jambo na hivyo kuutoa ili kuleta manufaa.
Kwa njia hiyo, wanajikuta wakiongea mambo muhimu na yenye tija kwao na kwa wengine.

Kabla ya kusema au kuandika chochote, hebu jiulize nini msukumo wako wa ndani wa kufanya hivyo?
Je unafanya ili uonekane na wewe upo? Au unafanya kwa sababu kuna kitu muhimu ndani yako unachotaka kukitoa?

Ni bora kukaa kimya kuliko kusema hovyo.
Kwa sababu wanasema hata mpumbavu akikaa kimya, anaweza kudhahiwa ni mwerevu.
Watu wengi wamekuwa wanaanika upumbavu wao hadharani kwa kuwa waongeaji sana.

Ili mawasiliano yakamilike na kuwa na tija kwa pande zote mbili, lazima yakamilishe lengo mahususi.
Tofauti na hapo mawasiliano yanageuka kuwa kelele zinazowakera watu.

Ukiwa mtu wa kuongea kwa sababu unaona na wewe inabidi uongee, utawachosha watu na wataacha kukuzingatia, kwa kuona huna jipya.
Lakini ukiwa mtu wa kuongea kwa sababu una kitu muhimu cha kuchangia, watu wanakusikiliza kwa umakini mkubwa ili wanufaike.

Chagua kukamilisha mawasiliano yako kwa umuhimu na usahihi ili uweze kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako kupitia kuwanufaisha wengine na mawasiliano yako.

Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MWONGOZO WA MAISHA YA MAFANIKIO na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu uhakika wa kushinda au kushindwa. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2024/01/12/3299

Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kuongea kwa sababu una mchango muhimu na siyo ili uonekane na wewe upo.

Kocha.