3300; Ambacho huwezi kupata.

Rafiki yangu mpendwa,

Wakati tupo shule tulikuwa na usemi mmoja kwamba unapoenda kwenye sherehe au mtoko wowote unaohusisha chakula, basi unapaswa kula chakula ambacho ni tofauti na kile unachokula kila siku.
Kwa sababu hicho cha kila siku unajua utaendelea kula, hivyo ni bora kutumia fursa mpya kula tofauti.

Nimekuja kugundua huu pia ni mpango mzuri sana pale unapojihusisha na watu.
Unahitaji kujihusisha na watu ambao wanakupa kile ambacho huwezi kukipata wewe mwenyewe.
Hasa kwa wale ambao unaingia gharama kuwa nao, mfano wafanyakazi, haina maana kuwa nao kama wanakupa kile ambacho wewe mwenyewe tayari unafanya.

Sababu pekee ya kuwa na watu wa ziada ni wakuletee kile ambacho hakipo wakati hawapo.
Kama una watu na hakuna tofauti ya wakiwepo na wasipokuwepo, basi jua hao unawabeba tu, hakuna wanachochangia.

Kadhalika unapokuwa unaongea na watu, unahitaji kuchagua wale ambao wanakuambia vitu ambavyo ni vigeni kwako na siyo kurudia vile ambavyo tayari unavifikiria muda wote.
Kama kuna kitu kikubwa na cha tofauti unataka kufanya, tayari unajua jinsi ambavyo ni kigumu kufanya na hakiwezekani.
Huhitaji tena mtu wa kukuambia hayo, maana unayajua na kuyafikiria muda wote.

Unachotaka ni watu wanaoweza kukuonyesha jinsi ya kupata unachotaka licha ya ugumu wake.
Hao ndiyo watu wanaoleta kitu cha tofauti kwako na kuweza kuchangia wewe kupiga hatua za tofauti.

Tusikubali kutoa muda, fedha na umakini wetu kwa watu ambao hakuna kipya wanachotuletea.
Wale ambao wanasema ambacho tayari unakifikiria na kufanya ambacho tayari unafanya, wanakuongezea tu mzigo usiokuwa na tija.

Kitu kimoja unachopaswa kujua ni kwamba watu huwa wanakuja na changamoto zao mbalimbali, ambazo lazima zitakuathiri.
Sasa kama kuna athari utakazopata, lazima hilo lifidiwe na vitu vya tofauti ambavyo watu hao wanakuletea.
Kama havipo, ni kujibebesha mzigo bure.

Ni lazima kila mtu unayempa nafasi kwenye maisha yako apambane kuthibitisha kwamba kuna thamani ya ziada anayoleta.
Nje ya hapo ni kuachana na watu na kutowapa nafasi kabisa.

Unapopewa nafasi, kuwa na mchango wa kipekee, ambao mtu hana.
Fanya hilo mapema ili watu wasiwe na mahangaiko ya kutafuta wengine wanaoweza kuwapa thamani ya tofauti.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe