💯KCM2324076; Kukufanyia.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#JumamosiYaUtulivu
Mwanamafanikio,
Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.
Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

💯 Neno la leo; Kukufanyia.
Leo ikiwa ni #JumamosiYaUtulivu tunaona jinsi ambavyo hakuna wa kukufanyia yale ya msingi unayopaswa kufanya kwenye maisha yako.
Siri kuu ya maisha ipo kwenye kuzaliwa na kwenye kifo.
Ulizaliwa peke yako na utazikwa peke yako.
Hata kwa waliozaliwa mapacha, bado kila mmoja anatoka kwa wakati wake na kuna namna anakuwa tofauti.
Na kwa wale wanaofariki kwenye janga linalohusisha wengi na kuzikwa makaburi ya pamoja, bado kutakuwa na alama ya kila mtu.
Hivyo tunachojifunza hapo, siri ya maisha ni upweke.
Uko peke yako kwenye hii safari, na ni wewe pekee unayepaswa kuikamilisha safari yako.
Wengine wanaweza kuambatana na wewe kwenye safari yako, lakini hakuna atakayeikamilisha safari kwa niaba yako.
Hicho ni kikombe chako, ambacho hakuna namna unaweza kukikwepa.
Watu wengi wamekuwa hawafanikiwi kwenye maisha yao kwa sababu wanategemea wengine kuikamilisha safari kwa niaba yao.
Wanachoambulia ni kushindwa na kupoteza muda na rasilimali nyingine.
Wengine pia wamekuwa wanakata tamaa pale wanapokosa wa kuwaunga mkono kwenye kile wanachotaka kupata.
Wanaona kwa kuwa hakuna mwingine anayewaunga mkono basi wanachotaka siyo sahihi.
Wanachosahau ni kwamba hakuna mwingine anayeona kile wanachoona wao.
Hivyo wajibu wao ni kukamilisha kile wanachoona kwa sababu ni cha kipekee kwao.
Jua kabisa kwamba safari kuu ya maisha yako ni safari ya upweke.
Na ili uweze kukamilisha safari hiyo ni lazima uweze kuwa na utulivu mkubwa wa kukuwezesha kukabiliana na kila kinachokuja mbele yako.
Pale unapokosa wa kukuunga mkono usikate tamaa, jua ni wewe unayeona unachoona.
Na hata unapopata wa kukuunga mkono au kukusaidia, kumbuka hawapo pale kwa ajili ya kufanya kwa niaba yako, ni wewe pekee unayepaswa kufanya, wao wanakuwa na mchango tu.
Ukijua hili mapema na kulizingatia, huwezi kuwa na lawama kwa mtu yeyote yule.
Kwa sababu utajua hakuna anayeweza kukamilisha wajibu wako mkuu zaidi yako mwenyewe.
💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MWONGOZO WA MAISHA YA MAFANIKIO na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu ambacho huwezi kupata. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2024/01/13/3300
Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kutekeleza wajibu wako mkuu kwa sababu hakuna atakayefanya kwa niaba yako.
Kocha.
💯