💯KCM2324077; Uwezekano.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#JumapiliYaMapumziko
Mwanamafanikio,
Mwaka huu wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kuweka umakini wetu wote kwenye kitu kimoja mpaka kitupe matokeo makubwa.
Na tunaachilia breki kupitia kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kuweza kupiga hatua kubwa.

💯 Neno la leo; Uwezekano.
Leo ikiwa ni #JumapiliYaMapumziko tunaangalia jinsi ambavyo siku hii ni ya kuangalia uwezekano usio na ukomo wa wiki iliyo mbele yako.
Pale watu wanapokuwa wanakimbizana na maisha, bila kupata nafasi ya kutulia na kutafakari, huwa wanajikuta wanarudia vitu vile vile ambavyo wamekuwa wanafanya na kuishia kupata matokeo yale yale.
Lakini ukweli ni kwamba kila mtu ana uwezo mkubwa na usio na ukomo mbele yake.
Uwezo huo hauwezi kuwa na manufaa kwa mtu kama haujafanyiwa kazi.
Na mtu hawezi kufanyia huo uwezo wake kazi kama hajui hata kama upo.
Kuwa na siku kwenye wiki ambayo unatafakari na kutathmini mwenendo wako mzima inakufungua sana kuweza kuuona huo uwezo na jinsi ya kuutumia.
Hiyo ndiyo kazi kuu ya siku ya jumapili na ndiyo maana ni muhimu kuifanya kuwa siku ya mapumziko.
Kupumzima huko siyo kuwa mvivu, bali ni kuhakikisha unachofanya unakifanya kwa usahihi na tija ili kupata unachotaka.
Hata mtu anayekata mti kwa shoka, kila baada ya muda anahitaji kuacha kukata na kunoa shoka lake.
Kuacha kwake kukata hakupunguzi matokeo, bali kunayaongeza kutokana na shoka kuwa limenolewa na makali yake kuwa mazuri.
Kila jumapili ifanye kuwa siku ya kunoa shoka lako, kwa kutafakari na kutathmini mwenendo wako mzima.
Kuangalia yale ambayo umeshafanya na uwezekano mkubwa ulio mbele yako.
Kuona na kujua ni nusu ya kupata, kwani unakuwa na njia sahihi ya kufanya ili upate unachotaka.
Unapoifanya jumapili kutokuwa ya kazi kama zilivyo siku nyingine za wiki, hupunguzi uzalishaji na ufanisi wako, bali unauongeza maradufu.
Kwa sababu unakuwa umeona njia bora za kufanya ili kupata matokeo yaliyo bora zaidi.
💯Hatua za kuchukua leo;
1. Leo ni siku ya mapumziko, wiki nzima umepambana kwa siku 6, siku hii ya 7 tenga muda wa kupumzika ili kukusanya nguvu za kuendelea na mapambano kwenye wiki nyingine.
2. Kamilisha mambo yako binafsi ambayo yalikwama kwa wiki nzima kutokana na kutingwa na shughuli zako za kikazi au kibiashara.
3. Tenga muda wa kupitia wiki unayomaliza na kupangilia wiki inayokwenda kuanza. Angalia yapi umefanya vyema na yapi ya kuboresha. Kisha panga matokeo unayotaka kuzalisha wiki inayofuata.
4. Fanya tathmini yako ya kazi/biashara kwa wiki uliyomaliza. Tathmini hii ihusishe namba muhimu ambazo unajipima nazo kwenye kile unachofanya. Tathmini inakuonyesha hatua ambazo umeshapiga na zile za kuendelea kupiga.
5. Tenga muda wa kutosha kwa watu muhimu kwako ili kujenga na kuimarisha mahusiano yako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kuonekana, kupata na kukosa. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2024/01/14/3301
Ukawe na siku bora kabisa ya mapumziko leo, siku ya kutafakari na kutathmini uwezekano mkubwa na usio na ukomo ulio mbele yako ili kuweza kuutumia kupata unachotaka.
Kocha.
💯