KCM2324078; Ung’ang’anizi.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#JumatatuYaMalengo

Mwanamafanikio,

Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.

Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

0678 977 007 kupata vitabu

 Neno la leo; Ung’ang’anizi.

Leo ikiwa ni #JumatatuYaMalengo tunaona jinsi ambavyo Ung’ang’anizi unahitajika ili kuweza kupata chochote unachokitaka kwenye maisha yako.

Huwa tunatamani maisha yangekuwa rahisi na tukaweza kupata kila tunachotaka bila ya kuteseka.
Lakini sivyo uhalisia wa maisha ulivyo.
Maisha ni magumu na yenye changamoto za kila aina.
Kupata chochote ambacho mtu unakitaka, lazima uwe na ung’ang’anizi wa hali ya juu sana.

Lazima uwe tayari kuendelea kufanya licha ya magumu na changamoto unazokutana nazo.
Lazima uwe tayari kuanza upya baada ya kuanguka na kupoteza kila kitu.
Siyo safari rahisi, lakini ni ambayo inawezekana kabisa.

Kufikia malengo yoyote uliyonayo, kuweza kutumia kile hasa kilocho ndani yako, ni lazima upambane sana.
Haijawahi kuwa rahisi na ndiyo maana wengi wamekuwa hawapati mafanikio wanayotaka.
Siyo kwa sababu mafanikio hayo hayawezekani, ila kwa sababu hawang’ang’ani vya kutosha.

Ukishaamua nini unachotaka, hapo kuwa umekata shauri na wewe mwenyewe kwamba lazima ukipate, liwake jua au inyeshe mvua.
Amua kwamba utapambania kile unachotaka mpaka ukipate bila ya kukubali kukwamishwa na chochote.

Ni maamuzi hayo ya kujitoa na kung’ang’ana ndiyo yatakayokuhakikishia kupata chochote unachotaka.
Unapokutana na ugumu wowote, usione kama ndiyo mwisho wa safari, bali jua ndiyo safari imekolea.
Kwani ukivuka hayo magumu, unakuwa umejisogeza karibu zaidi na lengo ulilonalo.

Hatupaswi kuomba mambo yawe rahisi, kamwe hayatakuja kuwa.
Tunachopaswa ni kuwa imara kiasi cha kuweza kukabiliana na ugumu wowote tunaokutana nao.
Ni uimara huo ndiyo unaotuwezesha kung’ang’ana bila ya kukata tamaa na kuacha.

Kifo cha ndoto kubwa za walio wengi ni kukata tamaa pale wanapokutana na magumu.
Wewe epuka hilo kwa kuwa na ung’ang’anizi usiochoka mpaka umepata unachotaka.

Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MWONGOZO WA MAISHA YA MAFANIKIO na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kujidanganya kwenye fedha. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2024/01/15/3302

Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kung’ang’ana na kile unachotaka mpaka ukipate bila ya kukubaliana na magumu yoyote unayokutana nayo.

Kocha.