💯KCM2324080; Huruma.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

JumatanoYaUwajibikaji

Mwanamafanikio,

Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.

Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

💯 Neno la leo; Huruma.

Leo ikiwa ni #JumatanoYaUwajibikaji tunaona jinsi ambavyo kutafuta huruma ya wengine kwenye matendo yako kunakuweka kwenye hatari ya kukosa msaada pale unapokuwa unauhitaji sana.

Maisha yako hivi, matokeo yoyote unayoyapata, ni wewe mwenyewe umeyasababisha kupitia mambo uliyoyafanya au kushindwa kuyafanya.
Ni wewe mwenyewe ndiye umejizingua na kusababisha matokeo unayoyapata.
Hivyo unawajibika kwa kila kitu kwenye maisha yako, bila kujali wengine wamefanya au kushindwa kufanya nini.

Watu wengi hawapo tayari kuwajibika na maisha yao kwa namna hiyo.
Hivyo wanapopata matokeo ambayo siyo mazuri, huwa wanatafuta mtu wa kumlaumu na kumlalamikia kwa hayo matokeo waliyopata.
Na uzuri ni kwamba, watu wa kulaumiwa na kulalamikiwa huwa hawakosekani.

Na ili lawama zionekane ni za kweli, watu hutafuta sana huruma. Hutengeneza maigizo ambayo yanawafanya watu wengine waamini ni kweli wamekwamishwa na watu wengine.
Kwa maigizo na kugusa hisia za wengine kwa huruma, wanakubaliwa na kuaminika mwanzoni.
Lakini kadiri muda unavyokwenda na watu kuzidi kutafuta huruma, wanazoeleka na kuonekana jinsi wanavyokwepa uwajibikaji kwao wenyewe.

Hilo linawafanya wale waliokuwa wanawaonea huruma kuanza kuwapuuza kwa kujua ni watu wasiotaka tu kuwajibika.
Hivyo hata pale wanapokuwa wanahitaji msaada kweli, wanakosa wa kuwasaidia kwa sababu wameshazoeleka ni watu wasiowajibika.
Mbinu yao ya kutafuta huruma kwa wengine inakuwa haifanyi kazi tena na zaidi inakuwa imeharibu kuaminika kwako.

Kuepuka yote hayo chagua kuwajibika na maisha yako.
Kubali kwamba kila linalotokea kwenye maisha yako ni wewe umesababisha.
Shika hatamu ya maisha yako kwa kuchukua hatua sahihi kwenye kila jambo.
Na kamwe usilaumu au kumlalamikia yeyote juu ya matokeo unayopata.

Sifa za watu huwa zinasambaa haraka.
Kadiri unavyokuwa tayari kuwajibika kwenye kile unachofanya, ndivyo unavyoaminika na wengi.
Hilo litakupa kazi ya ziada ya kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yako, kitu ambacho kitafungua fursa kubwa zaidi kwako.

Kubali kuwajibika kwa kila kitu kwenye maisha yako bila ya kujali wengine wamekuwa na mchango gani na utaaminika na kuweza kusaidiwa na wengi zaidi.
Lakini kutaka huruma kwa kulalamika na kulaumu wengine, utazoeleka na kupuuzwa kadiri muda unavyokwenda.

💯Hatua za kuchukua leo;

  1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
  2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MWONGOZO WA MAISHA YA MAFANIKIO na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
  3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
  4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
  5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kukwepa kuwajibika. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2024/01/17/3304

Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kuacha kutafuta huruma ya wengine kwenye matendo yako mwenyewe, chagua kuwajibika kwa kila kitu na utaweza kufanya makubwa.

Kocha.
💯