Mchakato wa mauzo ni sawa na mchezo wa mpira wa miguu. Mchezo huo huwa una chenga na magoli. Timu inapiga chenga ili iweze kufunga magoli.

Kuna timu inaweza kuwa inapiga chenga nzuri sana na kumiliki mpira kwa kiasi kikubwa, lakini ikashindwa kufunga magoli na hivyo kushindwa. Hiyo ni kwa sababu ushindi unahesabiwa kwa magoli yaliyofungwa na siyo chenga zilizopigwa.

Kwenye mauzo, mchakato mzima wa kumpata mteja na kumshawishi anunue ni chenga. Magoli ni pale mteja anapokamilishwa, yaani kukubali kununua kile anachoshawishiwa kununua.

Changamoto ambayo wauzaji wengi wamekuwa nayo ni kufanya vizuri mchakato mzima wa mauzo, lakini inapofikia kuwataka wateja wakamilishe mauzo, wanakwama. Ni kama wanapiga chenga nzuri sana, lakini wanapofika kwenye goli, wanatoa mpira nje badala ya kufunga.

Kukamilisha mauzo, yaani kumtenganisha mteja na fedha zake ndiyo kufunga magoli kwenye mauzo, ndiyo ushindi unavyohesabiwa. Ubaya wa mauzo ni hakuna sare wala nafasi ya pili, ni umeshinda (umeuza) au umeshindwa (umeuziwa). Kwenye mazungumzo yoyote ya mauzo, lazima kuna mtu atauziwa. Kama utamshawishi mteja akanunua basi unakuwa umeuza. Lakini kama mteja atakushawishi na kutonunua, anakuwa amekuuzia.

Kitu kikubwa kinachohitajika ili mtu kukamilisha mauzo ni ujasiri wa kumtenganisha mteja na fedha zake. Kwani mtu anakuwa tayari kukamilisha mchakato wote ila anashindwa mwishoni, hiyo ni kwa sababu ya mtazamo hasi na hofu anazokuwa nazo.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeshirikisha jinsi ya kujijengea ujasiri wa kukamilisha mauzo kwa kubadili mtazamo unaokuwa nao na kuondokana na hofu zinazokuzuia kuwatenganisha wateja na fedha zao. Karibu usikilize kipindi hicho hapo chini na ukafanyie kazi ili kuwa muuzaji bora.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 2. KISIMA CHA MAARIFA, 3. CHUO CHA MAUZO na 4. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.