💯KCM2324085; Kinachokukwamisha.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#JumatatuYaMalengo

Mwanamafanikio,

Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.

Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.



💯 Neno la leo; Kinachokukwamisha.

Leo ikiwa ni #JumatatuYaMalengo tunaona jinsi ambavyo kinachokukwamisha kufikia malengo yako ni wewe mwenyewe.

Pale watu wanaposhindwa kupata kile hasa walichotaka, huwa wanatafuta sababu.
Wanaanza kwa kuangalia ni watu gani wanaowazunguka ambao wanaweza kuwa wamewakwamisha.
Wakikosa kwenye watu wanaenda kwenye vikwazo vingine wanavyoweza kuviona kwenye mazingira waliyopo.
Wakikosa wanaangalia matatizo yanayoweza kuhusika kuwazuia.
Na kama kote watakosa, basi watasema wamekosa bahati.

Watu watazunguka sana kutafuta kinachowakwamisha, lakini hawatakuwa tayari kuukabili ukweli kwamba wao wenyewe ndiyo wanaojikwamisha.
Hakuna mtu au kitu chochote cha nje kinachoweza kumkwamisha mtu ambaye amejitoa kweli kweli kupata kile anachotaka.
Hata akutane na nini, atakuwa na namna ya kuvuka na kuendea kile anachotaka.
Lakini kama mtu hajajitoa hasa kupata kile anachotaka, anahitaji sababu kidogo tu aweze kuacha.
Hivyo kinachomkwamisha siyo hiyo sababu, bali ni kwa yeye mwenyewe kutokutaka hasa.

Kama watu wangekuwa wakweli kwao wenyewe na wakaacha kujidanganya kwenye mambo mengi, wangeweza kufanya makubwa sana.
Lakini kujidanganya na kujifariji kumekuwa kunawapoteza wengi.

Kupata chochote unachotaka kwa uhakika kabisa, jua unachotaka, weka malengo na mpango wa kukipata na fanyia kazi mpaka ukipate bila kukata tamaa au kuishia njiani.
Ukishindwa, jiambie ukweli ni wewe mwenyewe umechagua kujikwamisha badala ya kusingizia vitu vya nje visivyohusika.
Kuwa mkweli kwako mwenyewe ili ujiwajibishe na kuweza kupata chochote unachotaka.

💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MWONGOZO WA MAISHA YA MAFANIKIO na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kuokoa nguvu zako. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2024/01/22/3309

Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kuacha kujikwamisha wewe mwenyewe na kutafuta sababu za nje, jiwajibishe ili uweze kupata chochote unachotaka.

Kocha.
💯