Wote tunaujua usemi wa Kiswahili kwamba ahadi ni deni. Usemi huo unatufanya tujione tuna deni pale tunapowaahidi wengine na kuhakikisha tunatekeleza ili tuweze kuaminika.

Usemi huo una nguvu kubwa ya kukuza mauzo kwenye biashara kama ukiweza kutumiwa vizuri. Unachohitaji kwenye mauzo ni kuwashawishi wateja wakubali kununua, lakini wengi huwa hawapo tayari kununua kwa wakati ambao unawashawishi. Na hapo ndipo wengi hukosa fursa ya kukuza mauzo, kwa kukubaliana na wateja pale wanaposhindwa kununua.

Kama muuzaji ambaye unataka kufanya mauzo makubwa, unapaswa kujua kwamba ni wajibu wako kuwashawishi wateja wakubali kununua. Kwa sababu kile ulichonacho ndicho ambacho wateja wanakihitaji sana ili kuboresha maisha yao. Hivyo kama kuna kitu kinawakwamisha kuchukua hatua ya kununua pale unapowashawishi, unapaswa kuhakikisha unapata kitu kingine muhimu kutoka kwao. Kitu hicho ni AHADI.

Kama mteja ameshindwa kufanya maamuzi ya kununua, basi hakikisha unapata ahadi yake ya hatua atakayochukua baadaye. Kama hawezi kufanya maamuzi sasa, mfanye akuahidi lini ataweza kufanya maamuzi hayo muhimu. Baada ya mteja kukupa ahadi, kinachofuata ni wewe kufuatilia hiyo ahadi bila kuchoka.

Unachofanya ni kufanya vile ambavyo mteja amekuahidi. Amekuambia nitafute jumatano ijayo, mtafute hiyo jumatano. Amekuambia mwezi ujao, fanya hivyo. Wajibu wako ni kufuatilia kile alichoahidi, kwa jinsi alivyoahidi, bila kuchoka. Ukiwa na ufuatiliaji wa ahadi kiasi hicho, lazima utauza kwa wateja wengi zaidi.

Wateja wengi huwa wanatumia ahadi kama njia ya kutoroka mauzo. Wanakuwa hawana mpango wa kununua, lakini pia hawana ujasiri wa kusema hapana. Hivyo wanachofanya ni kutoa ahadi hewa, wakijua wauzaji wengi siyo wafuatiliaji wa ahadi. Na hivyo wanakuwa wamekwepa hilo kirahisi.

Wewe usikubali wateja wakupoteze kwa uzembe wako mwenyewe. Kama hawajawa na ujasiri wa kukukatalia na kuamua kukuahidi, wewe fuatilia ahadi zao kama walivyoziweka. Wakikuahidi tena fuatilia, nenda hivyo kwa msimamo bila kuacha.

Kwa ufuatiliaji wa uhakika, wengi watafanya maamuzi ya kununua. Na wapo ambao wanakataa kununua kabisa. Lakini kwa ujumla unakuwa umepata manufaa. Wengi huwa hawapendi kufanya ufuatiliaji huu wa uhakika kwa kusema hawataki kuonekana wasumbufu kwa wengine. Lakini hakuna usumbufu wowote hapo, ni unafuatilia ahadi zao. Kama hawataki, wanapaswa kukuambia kuliko kukupa matumaini hewa.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza kwa kina jinsi ya kutumia ahadi ni deni kufanya mauzo makubwa zaidi. Karibu ujifunze kwa kusikiliza kipindi na kwenda kuchukua hatua mara moja ili kunufaika.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 2. KISIMA CHA MAARIFA, 3. CHUO CHA MAUZO na 4. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.