3313; Kwa nini juhudi zako hazizai matunda.

Rafiki yangu mpendwa,
Ukiwaangalia wale wanaoshindwa na wanaofanikiwa, huwezi kuona tofauti kubwa sana kwa nje.
Kwa sababu kama ni juhudi, wote wanaweza kuonekana wakiweka juhudi kubwa.
Tena wakati mwingine wanaoshindwa wataonekana wanaweka juhudi kubwa kuliko hata wale wanaofanikiwa.

Lakini bado juhudi hizo kubwa wanazokuwa wanaweka hazizai matunda. Hiyo ni kwa sababu juhudi wanazokuwa wanaweka zinakosa mwongozo sahihi wa kuleta matokeo makubwa.

Kuna vitu ambavyo watu huwa wanafanya na vinapelekea juhudi wanazoweka kutokuzaa matunda.

Kitu cha kwanza ni tabia ya kuahirisha mambo. Mtu anakuwa amepanga kabisa nini atafanya na kwa wakati gani. Lakini unapofika wakati wa kufanya, anaahirisha na kujiambia atafanya wakati mwingine.
Anaenda akiahirisha hivyo mpaka pale kitu kinapohitajika hasa ndiyo atahangaika kukifanya.
Hapo ndipo mtu ataonekana kuchapa kazi sana.
Kwa sababu anafanya kwa haraka kutokana na kutokuwa na muda wa kutosha, anafanya kwa kulipua na hapati matokeo mazuri.
Hivyo licha ya kuonekana akichapa kazi sana kwa nje, haileti tija kwa sababu ni vitu alipaswa kuwa ameshafanya muda uliopita.

Kitu cha pili ni njia za mkato. Watu huwa wanapenda kupata kile wanachotaka kwa urahisi. Hivyo wanatafuta na kutumia njia za mkato. Kwa kuwa njia za mkato huwa hazifanyi kazi, anakuja kulazimika kuanza kufanya upya kwa njia sahihi na ndefu. Muda wote anaokuwa amehangaika na njia za mkato anakuwa ameupoteza. Hivyo licha ya kuonekana akiweka juhudi kubwa, zinakuwa za upotevu tu na kukosa tija kwa mtu.

Kitu cha tatu ni kukosa nidhamu ya kufanya kwa usahihi mara ya kwanza kufanya. Wengi huwa wanajifanyia tu kile wanachofanya vile wanavyojisikia. Matokeo yake ni wanatengeneza makosa ambayo yanakuja kuhitajika kurekebishwa. Na kurekebisha kilichokosewa huwa ni kazi kubwa kuliko kufanya kitu kwa usahihi mara ya kwanza.
Hivyo juhudi zitahitajika kubwa, lakini matokeo yafakuwa hafifu kwa sababu juhudi zinaenda kwenye mambo yasiyokuwa sahihi.

Kama unataka juhudi unazoweka ziweze kuzaa matunda mazuri, kamwe usiahirishe unayopanga, epuka njia za mkato na kuwa na nidhamu ya kufanya kitu kwa usahihi mara ya kwanza kukifanya.
Kwa kuzingatia hayo, kila juhudi unayoweka itazalisha matokeo makubwa na kukupeleka kwenye mafanikio makubwa unayoyapambania.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe