Kama umekuwa unafanya shughuli yoyote ya kukuingizia kipato, kwa muda mrefu lakini bado hujaweza kujenga utajiri ni kwa sababu huzijui sheria za fedha au kama unazijua basi unazipuuza.
Hivyo ndivyo moja ya vitabu bora kabisa kwenye eneo la fedha binafsi, THE RICHEST MAN IN BABYLON kinavyoeleza. Hiki ni kitabu kilichoandikwa karibu miaka 100 iliyopita na mpaka leo kinasimama kama msingi wa kujenga utajiri.

Kitabu hicho kina misingi saba muhimu ya mtu kufuata ili kujenga utajiri kwenye maisha yake. Msingi wa kwanza kabisa ukiwa ni kujilipa wewe mwenyewe kwanza kwa kutenga sehemu ya kila kipato unachoingiza.
Lakini pia kitabu kinazo sheria tano za fedha, sheria ambazo mtu asiyezifuata anaishia kutengana na fedha anazozipata. Na moja ya sheria hizo ni kuepuka kuwekeza fedha zako kwa tamaa ya kupata faida kubwa na ya haraka.
Kitabu kina hadithi nyingi ambazo zinakufanya msomaji kuelewa dhana zilizofundishwa kwa kina na kuweza kuzitumia kwenye maisha yako.
Moja ya hadithi hizo ni ya mtu aliyeuzwa kama mtumwa, lakini akajifunza falsafa nzuri ya maisha ambayo ni kupenda sana kazi. Kwa kupenda kwake kazi, aliweza kutoka kwenye utumwa na kujenga utajiri mkubwa.
Unaweza kudhani wewe siyo mtumwa, lakini nataka nikuambie kitu kimoja, kama hujafikia utajiri na uhuru wa kifedha, wewe ni mtumwa, bila kujali unajiona huru kiasi gani. Kama umeajiriwa na mshahara ndiyo chanzo chako pekee cha kipato, wewe ni mtumwa. Kama unafanya biashara na usipokuwepo basi biashara haiwezi kwenda, wewe ni mtumwa.
Kuanzia kwenye utumwa inaweza isiwe kosa lako, maana kuna mambo yanaweza kukufanya ujikute kwenye utumwa. Lakini kubaki kwenye utumwa kwa maisha yako yote ni kuchagua wewe mwenyewe.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeshirikisha hadithi sita za msingi za kujifunza jinsi ya kujenga utajiri kutoka kwenye kitabu hicho cha THE RICHEST MAN IN BABYLON. Karibu ujifunze kwenye kipindi hicho na ukachukue hatua ili kujenga utajiri na kuondoka kwenye utumwa ambao upo kwa sasa. Kipindi kipo hapo chini.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 2. KISIMA CHA MAARIFA, 3. CHUO CHA MAUZO na 4. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.