Huwa kuna kauli kwamba kushukuru ni kuomba tena. Hiyo ni kwa sababu unaposhukuru unakuwa umethamini kile ulichopata na hivyo kuwa tayari kupata tena.

Kwenye maisha, watu wengi wanakwama kwa sababu wanakosa shukrani. Kwa kila jambo wanalokutana nalo kwenye maisha, huwa wanaangalia upande wa lawama zaidi kuliko kuangalia upande wa kushukuru.

Ukweli ni kwamba, kwa mtu yeyote ambaye yupo hai, tayari ana mambo mengi sana ambayo anaweza kushukuru kuwa nayo kwenye maisha yake, hata kama sivyo alivyotegemea.

Kuwa na watu wa karibu wanaokupenda na kukujali ni kitu kikubwa cha kushukuru kwenye maisha. Maana maisha bila watu wa karibu, ni ya upweke mkubwa. Kuwa na shughuli ya kukuingizia kipato ni kitu cha kushukuru, hata kama siyo kiasi cha kipato ulichokuwa unataka kuingiza.

Lakini pia mambo yote ambayo umewahi kuyapitia kwenye maisha yako, mazuri na mabaya yana mchango mzuri kukufanya uwe hapo ulipo sasa. Hivyo unapaswa kushukuru kwa hayo yote uliyoyapitia.

Njia nzuri ya kushukuru siyo kusema tu unashukuru, bali kusema wazi nani au nini unachoshukuru na kwa sababu gani. Na hilo tunajifunza kwa mwanafalsafa wa Ustoa, Marcus Aurelius ambaye kwenye kitabu chake cha Meditations ameanza kwa kuorodhesha watu anaowashukuru na mchango ambao wamekuwa nao kwenye maisha yake. Amewataja watu kwa majina kabisa na kueleza nini ambacho amejifunza kwao, kitu ambacho kinatupa mengi ya kujifunza pia.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeshirikisha shukrani hizo za Marcus Aurelius na yale tunayojifunza kutoka kwenye hilo ili na sisi tuweze kufanya na kuwa na maisha bora. Karibu usikilize kipindi hiki na uende ukachukue hatua ya kuwa mtu wa shukrani ili uweze kupata zaidi na zaidi.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 2. KISIMA CHA MAARIFA, 3. CHUO CHA MAUZO na 4. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.