3316; Kwenye mafanikio, demokrasia haifanyi kazi.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki, mafanikio kwenye maisha yanahitaji uongozi.
Kuanzia uongozi binafsi mpaka kuwaongoza wengine.

Zipo aina mbalimbali za uongozi, lakini aina ambayo imekuwa inapewa nguvu zaidi kwenye zama hizi ni uongozi wa kidemokrasia.

Uongozi huo wa demokrasia huwa unatoa nafasi sawa kwa watu wote, bila kujali utofauti ambao upo kwa watu hao.

Hii ni aina nzuri ya uongozi kwenye mambo ambayo hayahitaji juhudi kubwa ili kupata matokeo makubwa.

Inapokuja kwenye kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha, hasa kwenye mambo binafsi, demokrasia haifanyi kazi.

Kujikubalia wewe mwenyewe kwa kila unachojiambia au kuwakubalia watu kwa sababu wana uhuru wa kuchagua ni nzuri kwenye nadharia, lakini kwenye vitendo ni kikwazo kikubwa.

Mafanikio makubwa yanakutaka mtu ujitoe sana, ujitese na kufanya zaidi ya ulivyo tayari kufanya.
Mafanikio makubwa hayajali sana kuhusu usawa wa haki kwa wote, bali unajali kujitoa sana kwa kila anayehusika.

Demokrasia ni kukubali kirahisi pale mtu unapotaka kutoroka kwenye njia ngumu. Ni kuwakubalia wengine wahangaike na mambo yasiyokuwa na tija na yanayowapoteza au kuwakwamisha kupata matokeo makubwa, kwa sababu tu wana haki ya kufanya hivyo.

Swali ni kama demokrasia haifanyi kazi kwenye mafanikio makubwa, aina gani ya uongozi inafanya kazi?
Jibu ni Udikteta Mwema.
Udikteta ni kujilazimisha wewe mwenyewe na kuwalazimisha wengine kufanya kitu ambacho kwa utashi wao wenyewe wanakuwa hawapo tayari kufanya.

Na udikteta unakuwa mwema pale kitu hicho unachojilazimisha kufanya au unachowalazimisha wengine kufanya, kina manufaa makubwa kwao binafsi.
Udikteta mbaya ni pale unapowatumia watu kwa manufaa yako binafsi, huku wao wakiumia au kupoteza.

Kwa kuwa mafanikio makubwa ni magumu na yenye kila aina ya changamoto, huwa ni rahisi kwa watu kutafuta namna ya kutoroka.
Watu hutafuta sababu nzuri sana za kutoroka, ambazo kidemokrasia zinakuwa halali kabisa.
Lakini kwenye udikteta mwema haupokei sababu hizo, badala yake unamlazimisha mtu afanye na kuleta matokeo yanayohitajika.

Kiongozi ambaye ni dikteta mwema hawezi kupendwa, hasa mwanzoni. Ila anaheshimika kwa ile misingi anayokuwa anaisimamia, ambayo baadaye inazalisha matokeo makubwa.

Udikteta mwema unapaswa kuanzia kwa mtu binafsi, usiwe rahisi kujishawishi kuiacha njia ya mafanikio kwa sababu ni ngumu. Endelea kukaa kwenye safari hiyo na pokea kila aina ya mateso mpaka utakapopata kile unachotaka.

Na pia unapaswa kutumia udikteta mzuri kwa wale unaowaongoza, kuanzia kwenye mambo binafsi mpaka kwenye shughuli mbalimbali unazofanya. Mkishakubaliana kitu cha kufanya, ambacho ndiyo sahihi kufanya, kinatakiwa kufanyika, hakuna kujadiliana katikati ya safari kuhusu kubadili kwa sababu ya ugumu ambao mmekutana nao.

Udikteta mwema unaleta mafanikio makubwa, lakini unapaswa kusimamiwa vyema ili uwe na manufaa kwa wote wanaohusika.

Rafiki, KISIMA CHA MAARIFA kinaendeshwa kwa mfumo wa Udikteta Mwema.
Tumejaribu sana mfumo wa demokrasia, kwa kutoa maarifa na kuwaacha watu wajiamulie wenyewe namna ya kufanya, lakini imekuwa haifanyi kazi.
Kwani watu wanaishia kujivuruga na kujikwamisha wao wenyeye.

Hivyo tunakwenda kusimama na Udikteta mwema bila kificho cha aina yoyote ile.
Kuchagua kuwa kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA maana yake umechagua kuuishi mchakato wake kamili, kama ulivyo, bila ya kuyumba kwa namna yoyote ile.

Mchakato mkuu wa KISIMA CHA MAARIFA ni MAARIFA + VITENDO = MAFANIKIO.
Unapata maarifa sahihi,
Unachukua hatua za tofauti,
Na kupata mafanikio makubwa.
Tunafanya hayo yote kwa kushirikiana kwa karibu, ili kuleta uwajibikaji wa pamoja.
Ushirikiano unaanza kwa jamii nzima ya KISIMA CHA MAARIFA kwenye kundi kuu la jamii hii.
Halafu unaendelea kwenye klabu ya KISIMA CHA MAARIFA kwa kukutana pamoja.

Ni lazima kupata MAARIFA na kila siku kushirikisha maarifa uliyopata.
Ni lazima kuchukua HATUA za tofauti na kila siku kushirikisha hatua hizo.
Na ni lazima upate MATOKEO ambayo utayashirikisha.
Lazima ufuate taratibu nyingine mbalimbali zilizopo kwenye jamii hii ya KISIMA CHA MAARIFA kwa sababu nia yake ni kuhakikisha kila aliye kwenye jamii hii anapata mafanikio makubwa kadiri ya anavyotaka.
Kwa sababu inawezekana, japo siyo rahisi.

Karibu rafiki kwenye udikteta wa kuchagua, kwenye mateso ya kujitakia, lakini utakaokuletea mafanikio makubwa ambayo hutaweza kuyapata kwa namna nyingine.

Kweye maoni hapo chini, shirikisha ULICHOJIFUNZA na HATUA UNAZOKWENDA kuchukua kwenye hii safari ya mafanikio.
Ni LAZIMA kushirikisha haya, siyo kama ukijisikia au ukipata muda, ni kufanya, kama maelekezo yalivyo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe