Kitu kimoja kuhusu sisi binadamu ni jinsi ambavyo huwa tuna uchaguzi wa wale ambao tunataka kujihusisha nao. Huwa tunaweka ni sifa za aina gani ambazo tunazitaka kwa watu tunaowahitaji kwenye maeneo mbalimbali.

Huwa inaanzia kwenye uchumba, mtu hueleza dhahiri anataka mchumba wa aina gani, mwenye sifa gani. Inaenda kwenye ushirika kwenye maeneo mengine ya kazi na biashara, watu wanataja kabisa sifa wanazotaka. Kwenye kuajiri pia, waajiri wanakuwa na sifa, huku waajiriwa nao wakiwa na sifa za kazi wanayoitaka.

Pamoja na kuweka huko vigezo, wengi sana wamekuwa wanaishia kupata kile ambacho hakiendani na vigezo vyao. Yaani wanapata watu ambao siyo sahihi kwao, lakini kwa sababu hawana namna nyingine, inabidi tu wakubali walichopata. Kinachofuata ni watu kulalamika kwamba hakuna watu sahihi au watu sahihi hawapatikani.

Hii dunia ina watu zaidi ya bilioni 8, hivyo unadhani kwamba katika wote hao watu sahihi wanakosekana? Nadhani unapata picha ya tofauti unapojiuliza swali hilo. Kwamba kwa wingi wa watu waliopo duniani, kwenye bara, nchi, mkoa, wilaya na hata mtaa, kuna watu sahihi wanaopatikana.

SOMA; 1936; Anza Na Watu Sahihi…

Kinachokuzuia usipate watu sahihi ni vitu viwili; moja ni wewe mwenyewe siyo sahihi na mbili unakubali wale wasio sahihi kwa kukosa uvumilivu.

Kwa maana hiyo basi, ili upate watu sahihi kwenye maisha yako, kwanza unatakiwa wewe mwenyewe uwe sahihi, kwa kuhakikisha zile sifa unazozitaka kwa wengine, kwako pia zipo. Halafu unatakiwa kuwa na subira na uvumilivu, usikate tamaa haraka kwa sababu watu unaokutana nao siyo sahihi, endelea kuwatafuta watu sahihi na utawapata. Na hilo litakuwa uhakika kama tu wewe mwenyewe utakuwa sahihi.

Kitu kimoja kitakachokushangaza sana ni kwamba pale unapoanza kuwa na sifa za watu unaowataka, utaanza kuwaona wakija kwako kwa wingi. Yaani utadhani kama walikuwa wamefichwa mahali na sasa wamefunguliwa. Kumbe kilichokuwa kinakuzuia ni ile hali ya wewe kukosa tabia unazotaka kwa wengine.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimefafanua hili kwa kina, angalia na ujifunze ili uanze wewe kuwa bora na kuweza kuwavuta watu bora kuja kwako.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.