Habari Wauzaji bora kuwa kutokea,
Tunachojua na kuamini ni kwamba ili kuwa wauzaji bora, lazima kwanza tuwe watu bora. Hivyo kukazana kuwa bora kupitia kujifunza na kuchukua hatua kwenye maendeleo binafsi, ni hitaji muhimu la mafanikio kwenye mauzo.
Tabia zetu ni kiungo muhimu sana kwenye matokeo tunayoyapata kwenye maisha. Huwa kuna kauli inayosema huwa tunajenga tabia, kisha tabia zinatujenga. Hiyo inaonyesha ni jinsi gani tabia zina nguvu.
Wakati wa kujenga tabia huwa tunahitaji kuweka kazi kubwa. Lakini tabia ikishajengeka, kuiendeleza ni rahisi. Popote ambapo mtu upo sasa, kumechangiwa na tabia ambazo unazo.

Ili kufanikiwa kwenye mauzo, kuna tabia 10 ambazo unapaswa kujijengea. Kazana kwa kila namna uweze kujijengea tabia hizo kumi, kwani kwa kuwa nazo, mafanikio yako kwenye mauzo ni ya uhakika.
Hapa unakwenda kujifunza tabia hizo kumi na hatua za kuchukua ili kuzijenga na kunufaika nazo.
Tabia 10 za kufanikiwa kwenye mauzo.
1. Uaminifu usiotiliwa shaka kwa mara zote kufanya kile kilicho sahihi, kuwa mkweli na kutimiza yote anayoahidi.
Bila uaminifu huwezi kufanikiwa kwenye mauzo, kujidanganya wewe mwenyewe na kuwadanganya wengine kutapeleka kutokuaminika. Kwenye mauzo ukishakosa kuaminika basi unakuwa umepoteza kila kitu.
Hatua; Kuwa mwaminifu kwenye mambo yako yote.
2. Nidhamu ya hali ya juu kwenye utekelezaji wa majukumu na maisha kwa ujumla.
Kuwa na nidhamu kali kwenye mambo yote unayofanya, ukishapanga, fanya kama ulivyopanga. Usiwe mvivu wala mzembe wa kuahirisha mambo kila wakati.
Hatua; Jisimamie wewe mwenyewe kabla hata hujasimamiwa na mtu mwingine, jiweke kitimoto wewe mwenyewe pale unapokuwa hufanyi vizuri na uchukue hatua sahihi.
3. Shauku kubwa kwenye kila jambo ambalo anafanya.
Huwezi kufanikiwa kwenye mauzo kama huna shauku kwenye kila unachofanya. Shauku haipaswi kuwa pale tu unapokutana na mteja, bali kwenye kila kitu unachofanya, kuwa na shauku kubwa. Kuwa na msukumo mkali wa ndani wa kufanya kwa viwango vya juu sana kila unachofanya.
Hatua; Muda wote kuwa mtu mwenye shauku kubwa, na hiyo itaathiri kila unachofanya ikiwepo mauzo.
4. Uchapakazi mzuri kwa kutekeleza majukumu ya kazi kwa ufanisi mkubwa na ndani ya muda bila ya kuchelewesha au kuahirisha.
Kazi ndiye rafiki wa kweli, rafiki ambaye hawezi kukutupa kwa namna yoyote ile. Weka kazi kubwa kwenye mauzo, kuanzia kujifunza, kutafuta wateja, kuwafuatilia, kuwauzia, kuwahudumia na kuhakikisha unawapa thamani kubwa. usitafute njia ya mkato ya kufanikiwa kwenye mauzo, haipo kabisa. Weka kazi na utapata matokeo mazuri.
Hatua; Penda kazi na jitoe kweli kweli kufanya kazi, utafanikiwa.
5. Unga’ng’anizi kwenye mambo yaliyo sahihi na siyo kukata tamaa na kuishia njiani.
Ukishapanga kwamba unataka kitu, ng’ang’ana mpaka ukipate. Usiishie njiani kwa namna yoyote ile. Ukikutana na ugumu, utumie huo kupata unachotaka. Uzuri wa dunia ni kwamba, ukikataa kile usichotaka, unaishia kupata unachotaka. Kataa chochote ambacho hakiendani na mafanikio yako na utafanikiwa.
Hatua; Unachotaka ni mafanikio kwenye mauzo, usikubali kingine chini ya hapo.
SOMA; Tumia Kauli Ya Ahadi Ni Deni Kukuza Mauzo Yako.
6. Usikilizaji makini wakati wa kufanya mazungumzo na watu wengine ili kuwaelewa vizuri na kuchukua hatua sahihi.
Una masikio mawili na mdomo mmoja kwa sababu kuu moja, unapaswa kusikiliza zaidi kuliko kuongea. Kusikiliza kwa umakini kuna nguvu kubwa sana ya ushawishi. Hiyo ni kwa sababu utawaelewa wengine vizuri na kuweza kuwashawishi vyema.
Hatua; Mara zote sikiliza kwa makini na waelewe watu ili uweze kuwashawishi vyema.
7. Kujifunza endelevu mara zote ili kuendelea kuwa bora.
Kuna vitu vingi sana ambavyo hujui na hilo kukukwamisha kupata mafanikio unayoyataka. Hivyo unapaswa kupenda kujifunza na kufanya kujifunza kuwa zoezi la kudumu kwenye maisha yako. Kamwe usifike mahali na kuona umeshajua kila kitu na huhitaji tena kujifunza. Kila mtu, bila kujali amefanikiwa kiasi gani, bado ana vitu vingi vya kujifunza.
Hatua; Tenga muda wa kujifunza kila siku na tumia muda huo kujifunza, kisha weka kwenye matendo yale unayojifunza.
8. Ari ya kufanya kilicho sahihi kabla ya kuambiwa au baada ya kuambiwa mara moja.
Watu wasiotekeleza kile wanachoambiwa, huwa wanashindwa kwenye maisha. Wale wanaotekeleza kile wanachoambiwa huwa wanafanya vizuri. Ila ni wale ambao wanatekeleza kabla hata ya kuambiwa ndiyo wanaopata mafanikio makubwa sana. Je wewe upo kwenye kundi gani kati ya hayo matatu?
Hatua; Wewe kama muuzaji unajua nini unapaswa kufanya kwenye majukumu yako, yatekeleze kabla hata hujaambiwa na utapata mafanikio makubwa.
9. Kujali kile unachofanya na wengine ili kuzalisha matokeo bora na yenye manufaa kwa walengwa.
Usifanye tu kitu leo kwa sababu jana ulifanya, au kwa sababu ndivyo wengine wanataka ufanye. Jali kile unachofanya, kipende hasa. Wajali wengine, kwa kuanza na wateja wako, wapende na jione ukiwa na wajibu wa kuyafanya maisha yao kuwa bora. Hilo litakusukuma kufanya zaidi na kuweza kupata mafanikio makubwa.
Hatua; Penda mauzo na wapende wateja wako, mapenzi yana nguvu ya kujenga mafanikio makubwa.
10. Tabia njema kulingana na maadili sahihi ya jamii.
Usifanye chochote ambacho ni kinyume na sheria au maadili ya jamii inayokuzunguka. Kufanya mambo ya aina hiyo yatakuletea usumbufu ambao unaondoa umakini wako kwenye mauzo. Unachotaka ni umakini wako wote uwe kwenye mauzo na mengine yote kuachana nayo. Ukizingatia sheria na taratibu mbalimbali, utaepuka usumbufu unaokuondoa kwenye mauzo.
Hatua; Kuwa raia mwema kwa kufuata sheria na taratibu ili usiingie kwenye usumbufu unaokutoa kwenye mauzo.
Muuzaji bora, tabia hizi kumi zipo ndani ya uwezo wako kuzijenga. Weka kazi kwenye kujijengea tabia hizi na zitakupa mafanikio makubwa. Kujijengea hizi tabia ni kuchagua kuziishi kwa vitendo na kuwataka watu wako wa karibu wakusimamie na kukukumbusha pale unapokwenda kinyume na tabia hizo.
Unapoteleza kwenye kujenga tabia hizo, usikate tamaa na kuacha, badala yake rudi kwenye njia sahihi na utaweza kujijengea tabia hizo.
Jijengee tabia bora za mauzo ili uweze kuwa mtu bora na muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.