Pata picha mtu amenunua basi lenye uwezo wa kubeba watu 30, ila yeye analitumia kama usafiri wake binafsi wa kwenda kwenye shughuli zake na anapanda yeye peke yake tu. Utamshangaa sana mtu huyo, iweje ana basi lenye uwezo wa kubeba watu wengi, ila analitumia kwa usafiri wake mwenyewe.
Hivyo ndivyo hata wewe ulivyo, ndani yako una uwezo mkubwa sana, uwezo wa kufanya makubwa kuliko unavyofanya sasa, lakini umekuwa unashindwa kutumia uwezo huo. Unayaendesha maisha yako kwa kufanyia kazi sehemu ndogo sana ya uwezo mkubwa ulionao, huku sehemu nyingine ikiwa haitumiki kabisa.
Unaweza kujiuliza unashindwaje kutumia uwezo huo, wakati wewe binafsi unajiona ukiwa unajituma sana kwenye yale unayofanya. Ni kweli unajituma sana, lakini sehemu kubwa ya juhudi unazoweka zinapotea bure kwa sababu ya breki ambazo umeziweka. Yaani wewe mwenyewe kuna breki ambazo umejiwekea na zimekuwa kikwazo kikubwa kwako kupiga hatua kubwa.

Kwa bahati mbaya sana, mtu unakuwa hujui breki unazokuwa umejiwekea, hivyo unajiendea ukidhani kila kitu kipo sawa, kumbe unajikwamisha. Breki hizo zinaweza kuwa za mwili, akili, roho au hisia. Lakini zimekuwa na nguvu ya kumkwamisha mtu na kumzuia asifanye makubwa.
Ili uweze kufanya zaidi ya unavyofanya sasa na ujenge mafanikio makubwa kwenye maisha yako, lazima kwanza uachilie breki hizo ambazo zinakuzuia kufanikiwa. Zipi njia nyingi za kuachilia breki, lakini moja ambayo ina nguvu na kila mtu anapaswa kuitumia ni kufanya tahajudi au kama inavyojulikana kwa Kiingereza, Meditation.
Huenda umekuwa unasikia kuhusu tahajudi lakini huelewi ni kitu gani. Au umewahi kujaribu kufanya tahajudi lakini hukuweza kuwa na mwendelezo mzuri. Wengine hudhani tahajudi ni kitu cha kufanywa na watu wa jamii fulani au wa dini fulani. Lakini ukweli ni tahajudi ni dhana pana na ambayo ina manufaa kwa mtu yeyote anayeweza kuifanya kwa usahihi.
SOMA; Tumia Tahajudi (Meditation) Kufungua Uwezo Mkubwa Ulio Ndani Yako.
Tahajudi inamjengea mtu uwezo wa kudhibiti fikra zake na kuzielekeza kwenye kitu kimoja kwa muda mrefu bila kuyumba. Huwa ni kawaida ya mawazo kuruka ruka kutoka kwenye kitu kimoja kwenda kwenye kitu kingine. Kwa kufanya tahajudi, unayafanya mawazo yako kukaa kwenye kitu kimoja kwa muda mrefu. Ni uwezo wa kuweka mawazo kwenye kitu kimoja kwa muda mrefu ndiyo unamwezesha mtu kufanya makubwa sana.
Ukiweza kudhibiti mawazo yako, kwa kuyaweka kwenye kitu unachokifanya bila ya kuyumbishwa, utaweza kukifanya kwa ubora wa hali ya juu na kupata matokeo ya kipekee.
Hivyo ndivyo tahajudi ilivyo na nguvu ya kukuwezesha wewe kufikia na kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yako.
Tahajudi ya kuachilia breki zinazokuzia kufanikiwa imegawanyika kwenye sehemu mbili.
Sehemu ya kwanza ni kutumia pumzi kudhibiti fikra zako. Hapa unafanya zoezi la kuweka fikra zako kwenye pumzi zako. Unachofanya ni kuvuta pumzi kwa kina ndani huku ukihesabu mpaka kumi, kushikilia pumzi ukihesabu tena mpaka kumi na kuachilia pumzi ukihesabu mpaka kumi. Unarudia hivyo mara kumi. Wakati unaendelea, kama mawazo yako yatahama, usihangaike nayo, wewe rudi kwenye zoezi.
Sehemu ya pili ni kujiambia kauli chanya huku ukijenga taswira ya kile unachotaka kwenye fikra zako. Chochote unachotaka kufanya au kupata, jione kabisa kama tayari unakifanya au umeshakipata. Fanya hilo huku ukiwa na hisia za upendo na furaha kwamba tayari umeshapata unachotaka. Zoezi hili linaifanya akili yako ya ndani (subconscious mind) kuziona fursa sahihi kwako kupata kile unachotaka.
Unapaswa kufanya tahajudi hii angalau mara mbili kwa siku, asubuhi unapoamka na usiku kabla ya kulala. Pia unaweza kufanya wakati mwingine wowote kwenye siku yako. Siyo lazima sana uwe eneo muhimu au uwe na mkao muhimu. Ukiweza kupata eneo tulivu ambalo linakuepusha na usumbufu, unaweza kukamilisha tahajudi hii.
Anza kufanya tahajudi hii na kwa matokeo unayopata, karibu uyashirikishe kwenye maoni hapo chini.
Karibu pia usikilize kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo nimefafanua kuhusu tahajudi hiyo ya kuachilia breki. Kipindi kipo hapo chini.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.