Habari Matajiri Wawekezaji,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya uwekezaji, ambayo tunayaweka kwenye vitendo kwa kuongeza kipato, kudhibiti matumizi na kufanya uwekezaji wa muda mrefu.

Uwekezaji ambao tumeuchagua kuwa wa kwanza kwetu ni wa Mifuko ya pamoja ya uwekezaji, ambayo kwa Kiingereza inaitwa Mutual Funds.

Hii ni aina ya uwekezaji kwenye masoko ya mitaji ambapo kunakuwa na mfuko wa uwekezaji ambao unakusanya mitaji ya wawekezaji kisha wenyewe kufanya uwekezaji.

Kwa kukusanya mitaji ya wawekezaji wengi, mfuko unakuwa na mtaji mkubwa na kwa kuwa na wataalamu sahihi wa uwekezaji, unawekeza vyema na wawekezaji wananufaika.

Uwekezaji kupitia mifuko ya pamoja imekuwa njia sahihi ya wawekezaji wadogo na wale ambao kazi yao kuu siyo uwekezaji, kuweza kunufaika na uwekezaji.

Watu wengi wamekuwa wanakwamishwa kuwekeza kwa sababu hizo kubwa mbili; mtaji wao ni mdogo na hawana uelewa sahihi wa wapi wawekeze kwa manufaa. Kwa kipato kidogo ambacho watu wanakuwa nacho, wanajikuta wakitumia chote kwa sababu hakitoshelezi. Lakini kwa uwepo wa mifuko ya pamoja, ambayo inapokea mitaji midogo midogo, inakuwa ni fursa nzuri kwa kila mtu kuwekeza.

Kadhalika, kuchagua uwekezaji sahihi ni kazi kubwa. Inataka mtu awe na uelewa mkubwa na afuatilie soko wakati wote. Kwa kuwa watu wengi wana shughuli zao nyingine, iwe ni ajira au biashara, wanakuwa hawana muda wa kutosha wa kujifunza na kufuatilia uwekezaji kwa karibu. Hilo linawaweka kwenye hali ya kushindwa kujua ni uwekezaji gani wafanye.

SOMA; Sheria 10 Za Kujenga Utajiri Mkubwa Kupitia Uwekezaji Mdogo Mdogo.  

Mifuko ya pamoja ya uwekezaji inatatua changamoto hizo mbili na kuwa fursa nzuri kwa watu wote wanaotaka kufanya uwekezaji kukamilisha hilo bila ya kuzuiwa na chochote.

Lakini pia mifuko ya pamoja ya uwekezaji huwa inatoa fursa rahisi ya wawekezaji kuuza uwekezaji wao na kupata fedha. Kwenye aina nyingine za uwekezaji, mwekezaji anaweza kuwa na uwekezaji mkubwa, lakini anapokuwa na uhitaji wa fedha za haraka, anashindwa kuuza uwekezaji wake kwa haraka. Kwa sababu inamtaka asubiri mpaka apatikane mnunuaji. Mfano hisa, ukiweka sokoni kuuza, ni mpaka apatikane mnunuzi, kadhalika ardhi na majengo. Lakini kwenye mifuko ya pamoja mambo ni tofauti, unapotaka kuuza, mfuko unanunua uwekezaji wako na kukupa fedha, hivyo huhitaji kusubiri mpaka mteja apatikane. Utasubiri kwa kipindi ambacho mfuko umeweka wa kuchakata ombi lako.

Hiyo ni faida kubwa kwenye uwekezaji, kwa sababu wengi wanakuwa na thamani kubwa ya uwekezaji ila hawana ukwasi. Wanapopata changamoto inayowahitaji kiasi kikubwa cha fedha, wanajikuta wakisumbuka sana.

Pamoja na urahisi huu wa kuwekeza kwenye mifuko ya pamoja, haiondoi changamoto za uwekezaji ambazo zipo kwenye kila aina ya uwekezaji.

Changamoto ya kwanza ni riba au ukuaji mdogo wa aina hii ya uwekezaji. Kwa kuwa mfuko unaenda kuwekeza mitaji ya wawekezaji, na kwa kuwa kuna gharama za kuendesha mfuko, faida inayopatikana inalipa kwanza gharama za mfuko na kisha faida kurudi kwa wawekezaji. Hilo linapunguza faida ambayo wawekezaji wanapata.

Lakini pia mifuko hii huwa inafanya uwekezaji mkubwa kwenye masoko mengine ya mitaji, ambayo ni Hisa na Hatifungani. Hivyo pale uchumi unapoyumba na uwekezaji kuyumba, hata uwekezaji wa mifuko ya pamoja unayumba pia. Japo uyumbaji wake unaweza usiwe mkubwa ukilinganisha na aina nyingine za uwekezaji.

Kwa Tanzania, uwekezaji wa mifuko ya pamoja ipo mbalimbali, binafsi na inayosimamiwa na serikali. Mifuko ambayo imekuwepo kwa muda mrefu na inayotoa fursa nzuri za uwekezaji kwa watu wote ni ile inayosimamiwa na UTT AMIS.

Kwenye somo linalofuata tutaanza kuiangalia UTT AMIS kwa ujumla na kisha kuingia kwenye mifuko yake na kuona kwa nini tumechagua kwenda na uwekezaji huu kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU.

Kama bado hujawa kwenye programu ya NGUVU YA BUKU, ambayo ni programu maalumu ya kujifunza na kuwekeza kidogo kidogo kwa muda mrefu, tuma ujumbe sasa wenye maneno NGUVU YA BUKU kwenda namba 0678 977 007 na utapewa utaratibu wa kuingia kwenye programu hiyo.

Mjadala wa somo hili.

Kwenye maoni hapo chini, shirikisha majibu ya maswali yafuatayo kama ulivyoelewa kwenye somo;

1. Zipi faida za uwekezaji kwenye mifuko ya pamoja?

2. Zipi hasara za uwekezaji kwenye mifuko ya pamoja?

3. Kwa nini ni muhimu kwa kila mtu kuwekeza kwenye mifuko ya pamoja?

Shirikisha majibu ya maswali hayo kama sehemu ya kujifunza na kuelewa somo hili na kwenda kutekeleza yale uliyojifunza.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.