3317; Kuzuia uharibifu.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki, binadamu tuna roho ya uharibifu ndani yetu.
Pale kitu kinapokuwa kinaenda vizuri, huwa haturidhiki na mwenendo huo.
Hivyo tunatafuta namna ya kukiharibu.
Unaweza kushangaa kwa nini iko hivyo, lakini huo ndiyo uhalisia.
Ni uwepo wa roho hiyo ya uharibifu na madhara yake kwa watu ndiko kunafanya kazi kubwa ya uongozi kuwa ni kuzuia roho ya uharibifu isilete madhara kwa watu.
Hilo linaonekana wazi kwenye mifumo mbalimbali iliyopo kwenye jamii zetu.
Kazi kubwa ya wazazi ni kuzuia watoto wao wasijiue kabla hawajafika umri wa watu wazima.
Kwa sababu watoto huwa wanatengeneza kila namna ya kutaka kujiua, kupitia michezo mbalimbali ya hatari wanayokuwa wanajihusisha nayo.

Halafu ni kazi ya serikali kuzuia watu wazima wasijiue. Ndiyo maana kuna sheria mbalimbali zinazowekwa kuwazuia watu wasijiletee madhara. Mfano sheria ya kufunga mkanda ukiwa kwenye chombo cha usafiri, serikali imeweka mpaka faini ya kulipa. Kufunga mkanda ni kwa faida yako, lakini mara nyingi hutafanya mpaka ulazimishwe na sheria zilozopo.
Kuna mifano mingi ya watu ambao wameanzia chini, wakajenga mafanikio, halafu baadaye wakayaharibu mafanikio hayo wao wenyewe.
Hilo linakuwa linatokana na roho ya uharibifu inayokuwa ndani ya mtu.
Kutokana na uwepo wa roho hiyo ya uharibifu, inafanya kila mtu kuwa na kazi kubwa ya uongozi ambayo ni kuzuia roho ya uharibifu ndani yake na kwa wale anaojihusisha nao.
Unawajibika kujizuia wewe mwenyewe usilete uharibifu kwenye mambo yote unayojihusisha nayo.
Kwa sababu ni kwa uvivu na uzembe ndiyo unaharibu mambo mengi ambayo umeshayajenga na yana manufaa kwako.
Pia unalazimika kuwazuia wale wote unaojihusisha nao wasijiletee uharibifu wao wenyewe au kuharibu kile ulichojenga wewe.
Unahakikisha huruhusu mazingira yoyote ya uvivu au uzembe yaingie kwenye kile unachokazana kujenga.
Weka viwango vya juu sana ambavyo kila anayehusika anapaswa kupambana kuvifikia.
Usishushe viwango hivyo ili kuwaridhisha na kuwavutia watu, utaharibu kabisa kile unachojenga.
Bali simamia viwango hivyo ili wale walio sahihi wapambane kuvifikia na hapo utajenga kitu imara kitakachodumu kwenye mafanikio.
KISIMA CHA MAARIFA ni jamii ambayo inazuia kabisa uharibifu na kifo kwenye mafanikio.
Jamii hii ina viwango vya juu sana kwenye KUJIFUNZA endelevu na kuchukua HATUA za tofauti mara zote ili kupata MATOKEO bora sana.
Hakuna anayepata nafasi ya kubaki kwenye jamii hii kama hazingatii msingi huo mkuu wa MAARIFA + VITENDO = MAFANIKIO.
Ndani ya jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, chini ya uongozi wa Kocha Dr Makirita Amani ni marufuku kabisa kuwepo kwa uvivu au uzembe ambao unaathiri mafanikio yanayojengwa.
Adhabu kali ya kuondolewa kwenye jamii hii inatekelezwa kwa wote ambao hawapambani kufikia viwango vilivyowekwa.
Sababu na visingizio havina nafasi ya kusikilizwa.
Ni mtu anachagua kufanya au kutokufanya, mengine yote hayapewi nafasi kabisa.
Kama umechagua kuwa kwenye jamii hii, basi nenda kwa viwango hivyo.
Jenga mafanikio ambayo yatadumu kwa sababu unaepuka uharibifu na kifo.
Na wajibu wako ni mmoja tu, kufuata mchakato ambao tayari upo.
Usiyumbe kwa namna yoyote ile.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe