Karibuni wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea kwenye masomo ya mauzo eneo la usakaji. Kauli mbiu yetu kwenye usakaji ni USAKAJI NI PUMZI YA BIASHARA, UNAPASWA KUFANYIKA MARA ZOTE.

Kwenye masomo yaliyopita tuliona usakaji kwa njia ya kuwatembelea wateja na kukutana nao ana kwa ana. Tuliona jinsi ambavyo njia ya ana kwa ana ilivyo na ushawishi mkubwa kwa wateja.

Lakini pamoja na ushawishi huo wa ana kwa ana, bado wateja wengi utakaokutana nao kwa mara ya kwanza hawatakuwa tayari kununua au kukubaliana na wewe. Wanaweza kukusikiliza, lakini kama ndiyo mara ya kwanza wanakutana na wewe, siyo rahisi wakubali kuchukua hatua.

Wengi wanakuwa na wasiwasi kwa sababu wewe ni mgeni kwao. Ndiyo wamekuona, lakini bado wana hali ya wasiwasi, wanaona huenda ni tapeli unayepita tu kuwahadaa watu.

Hivyo mpango wako wa usakaji kwa kutembelea hauwezi kukamilika kama utakuwa unawafikia watu mara moja na kutokurudi tena. Badala yake unatakiwa kurudi kwa wote ambao umeshawapitia na kufanya hivyo mara kwa mara, iwe wamenunua au la.

Kuwarudia wateja mara kwa mara ndiyo ufuatiliaji. Na ufuatiliaji huwa una nguvu kwa sababu ya kuzoeleka. Mara ya kwanza kwa watu unakuwa mgeni. Unaporudi tena ugeni unapungua lakini hofu inakuwepo. Ukirudi tena hofu inazidi kupungua. Ukiwafikia watu zaidi ya mara saba, wanakuwa wamejenga imani kubwa kwako, kwa sababu hakuna tapeli au mtu mwenye nia mbaya anayeweza kurudi kwa watu mara nyingi kiasi hicho.

Unapopanga usakaji wako kwa njia ya kuwatembelea wateja, lazima uweke mipango hiyo miwili, kuwafikia wateja wapya kabisa ambao hawaijui biashara yako. Na pia kuwafikia wateja ambao tayari wanaijua, ambao wameshanunua au bado hawajanunua.

SOMA; Mkakati Mkuu Wa Usakaji Endelevu Kwenye Chuo Cha Mauzo.

Unapoenda kwa mteja kwa mara ya kwanza, nenda ukiwa chanya kwamba atanunua, lakini inapotokea hajanunua, usione kwamba huo ndiyo mwisho wa mchakato wako. Bali jua ndiyo mwanzo wa ufuatiliaji. Mweke kila mteja ambaye umeshamtembelea kwenye ratiba yako ya kurudi tena kumtembelea ili kuzidi kuzoeleka, kuaminika na hatimaye kufanya biashara.

Katika kuwafuatilia wateja kwa kuwatembelea, hakikisha unazingatia mambo haya;

1. Kuwa na ratiba nzuri ya kurudi kwa wateja kiasi kwamba wanaweza kukutegemea. Kama ni siku fulani ya wiki basi nenda kwenye siku hiyo hiyo. Unapokuwa na mazoea ya kuonekana kwa siku fulani, na ukafanya hivyo, unaaminika zaidi.

2. Kila unapomfuatilia mteja, kuwa na thamani unayoongeza kwake. Nenda kwake ukiwa na taarifa mpya ambazo haya, mshirikishe maarifa ambayo hana na hata kumsaidia vitu vinavyomtatiza ambavyo vipo ndani ya uwezo wako. Pia kwa maeneo ambayo unaona anakwama na una njia ya kumsaidia, fanya hivyo. Mfano kumuunganisha na watu wanaoweza kumpatia kitu anachotaka.

3. Kila unapomfuatilia mteja, kusanya taarifa zaidi kuhusu yeye. Angalia mazingira ya biashara yake, kazi yake au nyumbani kwake. Popote unapomkuta mteja, angalia mazingira yake. Kama ana picha za familia yake, jua anajali familia, hivyo jua majina ya watu wa familia yake, utaweza kuyatumia kwa ushawishi zaidi. Kama anavaa jezi za timu za mpira, ni shabiki wa mpira, jua timu anayoishabikia na uongee naye kuhusu hilo zaidi. Usitumie fursa ya kukutana na wateja na ukashindwa kukusanya taarifa nyingi zaidi ambazo baadaye utazitumia kwa ushawishi mkubwa.

4. Kila unapomfuatilia mteja, msogeze karibu zaidi na yeye kufanya maamuzi. Usiende tu kama unaenda kutembea, bali nenda ukijua nini hasa unaenda kukamilisha. Kwa mfano kama mteja huwa anakupa pingamizi fulani, kila unapoenda jipange kupangua pingamizi hilo ili aweze kuwa tayari kufanya maamuzi unayomshawishi afanye.

5. Wateja ambao umeshawaweka kwenye ufuatiliaji, wafuatilie kwa msimamo bila kuacha. Unachopaswa kufanya ni kubadili yale unayofanya kwenye kila ufuatiliaji unaofanya ili watu wasichoke na kuzoea. Kila mara wawe na mategemeo ya kupata kitu cha tofauti kutokana na ufuatiliaji wako. Badili pia maeneo unayokutana na wateja na hilo litazidi kuongeza kuaminika.

Wewe kama muuzaji bora kuwahi kutokea, unapokuwa unawatembelea wateja, jua siyo tukio la mara moja, bali ni mchakato endelevu. Panga kuwatembelea wateja kwa uendelevu ili uweze kunufaika nao kwa ukubwa. Unawafuatilia wateja mpaka wanunue na wakishanunua unaendelea kuwafuatilia ili waendelee kununua. Ufuatiliaji una nguvu kubwa pale unapofanyika kwa usahihi. Hakikisha unafanya ufuatiliaji wako kwa usahihi ili unufaike nao.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.