Mafanikio ni kitu ambacho kinapendwa na kila mtu, kwa sababu ndiyo udhihirisho kwamba mtu ameweza kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yake kufanya makubwa.
Lakini pia mafanikio ndiyo kitu kimekuwa adimu kwa watu wengi, licha ya kuyataka sana, licha ya kupambania, bado wengi wanabaki kwenye maisha ya kawaida.
Kuna mambo mengi yanayofanya watu wabaki kwenye maisha ya kawaida, licha ya kuwa na uwezo wa kufanya makubwa ndani yao.
Kitu cha kwanza ni kuishi kwa mazoea, hasa pale maisha yanapokuwa rahisi au mtu kuwa na utegemezi kwa watu wengine. Hili unaweza kuliona kwa watu waliozaliwa na kukulia eneo fulani, huwa hawafanikiwi kama wale waliohamia eneo hilo.

Kwenye maeneo mengi unakuta wageni wana mafanikio makubwa kuliko wenyeji. Hiyo ni kwa sababu wakati wenyeji wanaishi kwa mazoea na utegemezi kwa wengine, wageni wanakuja wakiwa wanajua hawana cha kutegemea bali kupambana. Ni mapambano hayo ndiyo yanayowapa mafanikio makubwa.
Mfano mwingine ni watu unaokuta wako kwenye ajira au biashara fulani ambayo inawatosheleza kuendesha maisha yao. Kwa kipindi kirefu wanakuwa na maisha ya kawaida. Lakini inatokea wanafukuzwa kazi au biashara inakufa na kulazimika kwenda kuanza vitu vipya, huwa wanafanikiwa zaidi kwenye vitu hivyo vipya. Ile hasira ya kukosa kitu walichokuwa nacho awali inawasukuma kufanya zaidi kwenye kitu kipya.
Unapata picha hapo kwamba kikwazo kikubwa cha mafanikio makubwa ni yale mazoea ambayo tayari mtu anayo. Na hapo ndiyo maana ubatizo wa moto unahusika, ambapo mtu anapitia hali fulani inayoharibu yale mategemeo aliyokuwa nayo.
SOMA; 7/30; Njoo upate ubatizo wa uhakika wa mafanikio.
Dhana ya ubatizo wa moto inaendana na mfumo wa hadithi wa safari ya shujaa. Huu ndiyo mfumo mkuu wa hadithi zote, ambapo shujaa anakuwa anaendesha maisha yake kwa kawaida tu. Halafu kinatokea kitu ambacho kinayavuruga kabisa maisha yake kiasi cha kushindwa kuendelea kama awali. Hapo ndipo maisha yanapobadilika kabisa na kuanza kufanya mambo makubwa na ya tofauti.
Lakini kwenye safari hiyo ya shujaa mambo huwa hayawi rahisi. Kwanza kabisa anakutana na magumu na changamoto ambazo kwa wengi zinakatisha tamaa, lakini kwa shujaa anazivuka kwa kuwa amedhamiria kweli kufanikiwa. Akishavuka hayo magumu siyo kwamba mambo yanakuwa rahisi, bali anakutana na vishawishi vya tamaa. Anaona vitu vizuri kwake kuhangaika navyo ambavyo ni tofauti na kile anachotaka. Vishawishi hivyo huwa vinawaangusha wengi, lakini shujaa anavuka. Kwenye safari pia shujaa anakuwa na menta anayemwongoza na anayejifunza kwake. Kwa kupambana hasa, anapata ushindi.
Kuna vitu vitatu tunavyoviona kwenye safari ya shujaa hapo, ambavyo vinakosekana kwa walio wengi na kuwa kikwazo kwao kufanikiwa. Vitu hivyo vitatu ndivyo vinapatikana kwenye ubatizo wa moto ambao unaleta mapinduzi makubwa kabisa kwa mtu.
Kitu cha kwanza ni kuweza kuvuka magumu na changamoto. Lazima mtu awe na ung’ang’anizi wa hali ya juu ndiyo aweze kupata kile anachotaka. Akiwa na roho nyepesi hataweza kufika mbali.
Kitu cha pili ni kuweza kuvuka vishawishi na tamaa. Wengi sana wameshindwa kupata mafanikio makubwa kwa sababu ya kuhangaika na vitu vinavyoonekana ni vizuri kwa nje, lakini kwa ndani havina manufaa makubwa kama mafanikio wanayopaswa kuyapambania. Kuna ambao wanaweza kuvuka magumu, lakini vishawishi vikawakwamisha.
Kitu cha tatu ni kuwa na menta ambaye mtu anajifunza kwake na hata kujipima naye kwenye safari yake ya mafanikio. Wengi sana hawana kipimo sahihi kwenye safari ya mafanikio, hivyo wanaweza kujiona wanafanya sana, lakini kiuhalisia hawafanyi kihivyo. Mtu anapokuwa na menta, anapata njia sahihi ya kujipima na kujisukuma kufanya makubwa.
Fanyia kazi haya mambo muhimu ya huu ubatizo, kuondoka kwenye mazoea, kuvuka magumu, kuepuka tamaa na kuwa na menta na utaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yako.
Karibu usikilize kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini kupata ufafanuzi zaidi kwenye dhana hii ya ubatizo wa moto kwenye mafanikio.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.