3321; Siyo ngumu kihivyo.
Kutoka mezani kwa Kocha.
Rafiki, safari ya mafanikio tayari ina ugumu wake.
Lakini cha kushangaza, watu huwa wanazidisha ugumu huo, kitu kinachowakwamisha kupiga hatua kubwa.
Hilo linafanya safari hiyo kuonekana ni ngumu sana na isiyowezekana kabisa.
Ugumu huo wa ziada unakuwa umesababishwa na mtu mwenyewe, kwenye vitu anavyokuwa amefanya au kushindwa kufanya.

Kwa sehemu kubwa, hii safari ya mafanikio inataka vitu viwili tu.
Kitu cha kwanza ni KUSEMA UTAFANYA KITU.
Hapa unatoa ahadi ya nini ambacho utafanya kwa wengine.
Kama ni kazi unasema kabisa nini unakwenda kufanya.
Kwa biashara, unamweleza mteja yale anayokwenda kupata.
Hiki ni kitu rahisi kufanya na wengi wanakifanya.
Wakati kufanya kitu hiki huwa inaonekana rahisi, lakini ndipo ugumu huwa unaongezeka kama kitu cha pili hakitafanyika.
Kitu cha pili ni KUFANYA ULICHOSEMA UTAFANYA.
Hapa unatimiza ahadi ambayo umetoa kwa wengine.
Unatekeleza yale uliyosema kwamba utafanya.
Na hapa ndipo ugumu zaidi huwa unatengenezwa.
Kama mtu atashindwa kutekeleza kama alivyoahidi, siyo tu anakosa alichotaka, bali pia anapoteza uaminifu.
Na hapo anaifanya safari yake kubwa ngumu zaidi, anakuwa hajapata alichotaja, lakini pia anakuwa haaminiki tena.
Kuahidi ni rahisi na watu huwa wanavutiwa kufanya hivyo, kwa sababu inaonekana ni njia ya mkato kuwashawishi wengine.
Hivyo watu huwa wanajikuta wanaahidi makubwa na kwa kujiamini, kitu kinachopelekea waaminike.
Kutekeleza ahadi ni ngumu na watu huwa wanatafuta visingizio mbalimbali kwa nini wameshindwa kutimiza.
Walioahidiwa lakini ahadi kutokutimizwa, wanaweza wakasikia sababu na visingizio vinavyotolewa, lakini wanakuwa hawana tena imani na mtu.
Sasa basi, hakuna kitu kigumu kuvuka kwenye safari ya mafanikio kama kutokuaminika, hasa kwa kushindwa kutekeleza ahadi zako mwenyewe.
Kila unapowaahidi tena watu kitu wanakuwa wanachukulia hutatimiza, kwa sababu hicho ndiyo umeshawaonyesha.
Kama hutaki kuongeza ugumu kwenye safari yako ya mafanikio, AHIDI NA TEKELEZA.
Hata kama unapitia nini, tekeleza bila ya sababu au visingizio vyovyote.
Kama tu upo hai, tekeleza kile ulichoahidi.
Hata kama itabidi ikutese na kukuingia gharama kubwa.
Jijengee sifa ya kuwa mtu wa kutekeleza kwa uhakika kila unachoahidi.
Lifanye neno lako kuwa sheria.
Wafanye wengine wakuamini bila ya shaka yoyote.
Ukiliweza hili, mafanikio kwako hayatakuwa magumu kihivyo.
Unakuwa na uwanja mpana wa kucheza na ambao hauna ushindani kwa sababu wengi wanaahidi ila hawatekelezi.
Kwenye KISIMA CHA MAARIFA, kila mwanachama ana ahadi yake kuu, ambayo ndiyo anayoipambania muda wote.
Ahadi kuu ndiyo lengo ambalo mtu anataka kulifikia na litakaloleta matokeo ya tofauti.
Wajibu wa kila mwanachama ni kuandika ahadi yake kila siku na kuweka kwenye kundi, kisha kuitimiza.
Lakini pia ndani ya KISIMA CHA MAARIFA unaaminika na kuendelea kupata nafasi pale unapokuwa mtu wa kufanya yale unayosema utafanya.
Hakuna anayekulazimisha ufanye chochote, ila ni wewe mwenyewe unaahidi ya kufanya, kisha unafuatiliwa kutimiza kama ulivyopanga.
Hakuna sababu wala kisingizio kitakachopokelewa pale unaposhindwa kufanya ulichosema utafanya.
Kitu pekee kitakachokuondoa kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA ni kushindwa kutekeleza yale unayoahidi.
Ukishakosa kuaminika, huwezi tena kupata nafasi kwenye jamii hiyo.
Rafiki, mafanikio siyo magumu kihivyo kama utaahidi na kutekeleza mara zote.
Zingatia hili kwenye maeneo yote ya maisha yako na utaona jinsi ambavyo safari itakuwa nyepesi kwako.
Kwa kuwa wengi hawafanyi hili, utajitofautisha sana na wengine na kuwavutia wengi kujihusisha na wewe.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe