3322; Kupata na kukosa.
Kutoka mezani kwa Kocha.
Inawezekana kabisa kutengeneza vyombo vya usafiri, ambavyo hata ikitokea ajali, watu hawawezi kupata madhara kabisa.
Lakini sasa, vitakuwa vikubwa sana na vizito mno kiasi kwamba havitaweza kuwa na mwendo unaohitajika ili kukamilisha safari kwa wakati.
Hivyo basi, kupata usalama zaidi kutasababisha kukosa kasi zaidi.
Ndivyo maisha yalivyo, kupata kimoja huwa kunapelekea kukosa kingine.

Watu wengi kwenye maisha wamekuwa wanajikuta njia panda na kukwama kuendelea kwa sababu wanataka kupata tu bila kupoteza.
Wakati uhalisia ni kupata vitu fulani, lazima uwe tayari kupoteza vitu vingine.
Hili limekuwa linawakwamisha watu kwenye kuongeza kipato.
Kwa sababu ongezeko lolote la kipato huwa linakuja na kupungua kwa uhakika wa kipato hicho.
Kwenye maisha ni unaweza kuwa na kipato kidogo cha uhakika au kuwa na kipato kikubwa kisichokuwa cha uhakika.
Ukipata uhakika unakosa wingi na ukipata wingi unakosa uhakika.
Kwenye safari ya mafanikio makubwa ambayo tupo, hupaswi hata kujiuliza mara mbili pale unapokuta kwamba inabidi ukose baadhi ya vitu ili upate vile unavyotaka.
Hilo unapaswa kulijua kabisa ili lisikukwamishe kwa namna yoyote ile.
Kupata unachotaka, lazima kuna vitu utavikosa.
Kadiri unachotaka kinavyokuwa kikubwa, ndivyo unachopoteza kinakuwa kikubwa pia.
Kubaliana na hali hiyo mapema ili uweze kupata unachotaka.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, tunapambana kujenga mafanikio makubwa sana.
Kitendo tu cha kuchagua hii safari, kuna vitu tumekuwa tayari kuvikosa, ambavyo watu wengine wananufaika navyo.
Tumekosa starehe ambazo wengine wanazipata.
Tumekosa usingizi ambao wengine wanaufurahia.
Tumekosa mahusiano ambayo wengine wanayo.
Tumekaribisha kukosolewa na kukatishwa tamaa kuliko wengine.
Tumekosa uhakika ambao wengine wanao.
Pamoja na hayo yote ambayo tumeyakosa, kile tunachopata ni kikubwa na muhimu zaidi kwetu.
Hivyo tunakuwa tayari kupoteza hivyo vingine vyote kwa ajili ya yale tunayoenda kupata.
Usikae ndani ya jamii ya KISIMA CHA MAARIFA halafu ukawa unajilinganisha na walio nje ya jamii hii.
Mwanzo utaona unajitesa wakati wengine wanafurahia.
Lakini mbeleni, wakati wewe unafurahia, hao wengine watakuwa wanateseka.
Kaa kwenye mchakato wa KISIMA CHA MAARIFA, kuna vitu utavikosa kwa kukaa kwenye mchakato huo, lakini utakavyokuja kuvipata baadaye vitakuwa vikubwa kuliko hivyo ulivyokosa.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe