Swali la ni biashara gani inayolipa sana, ambayo mtu akiifanya atapata mafanikio makubwa na kwa uhakika ni swali ambalo limekuwa linaulizwa na watu wengi.
Wengi hudhani kwamba kuna siri fulani iliyofichwa juu ya mafanikio ya biashara. Kwamba wale waliofanikiwa sana kwenye biashara, kuna namna walichagua biashara hizo ambayo ni tofauti na wale walioshindwa.
Huo ni ukweli kabisa, wanaofanikiwa kwenye biashara, kuna namna wanavyochagua biashara zao tofauti kabisa na wale ambao wanashindwa. Lakini sasa, ukiiga kile walichofanya wao wakafanikiwa, siyo uhakika kwamba na wewe utafanikiwa.

Hapo ndipo wengi huwa wanashindwa kuelewa na hilo kupelekea washindwe kufanikiwa kwenye biashara.
Siri kubwa ambayo wengi wamekuwa hawaijui kwenye mafanikio ya biashara ni kwamba; mafanikio ya biashara hayaanzii kwenye biashara, bali yanaanzia kwa yule anayeifanya biashara.
Kwa kuwa kwenye kila biashara kuna watu waliofanikiwa na walioshindwa, inathibitisha kwamba tatizo halianzii kwenye biashara, bali kwa wale wanaofanya biashara hiyo.
Hivyo unapouliza tena swali la biashara gani inalipa sana na ukiifanya itafanikiwa, usiulize kwa kuwaangalia wengine, bali uliza kwa kujiangalia wewe mwenyewe.
Hiyo ina maana kwamba biashara ambayo wengine wanafanya na wakafanikiwa, wewe unaweza kuifanya na usifanikiwe. Siyo kwa sababu biashara hiyo haina mafanikio, bali kwa sababu inaweza kuwa haiendani na wewe.
Ili uweze kupata mafanikio makubwa kwenye chochote unachofanya, lazima uwe na vipaji au uwezo fulani ambao wengine hawana, unaokuweka mbele kwenye kitu hicho. Lazima uweze kuleta matokeo ya tofauti na wanayoleta wengine, licha ya kuwa mnafanya kitu kimoja.
Hiyo ndiyo sababu ni muhimu sana mafanikio yoyote unayoyafikiria, yaanze na wewe kabla ya kuwaangalia watu wengine. Kwa kuchagua biashara ambayo inaendana na wewe, ambapo unaweza kufanya vitu vya tofauti na hata kung’ang’ana nayo kwa muda mrefu kuliko wengine, mafanikio yanakuwa yako kwa uhakika.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza kwa kina jinsi ya kuchagua biashara ambayo ni sahihi kwako wewe kuifanya. Karibu usikilize kipindi hicho ili uweze kuanzisha biashara sahihi kama bado hujaanza au kuboresha ile ambayo umeshaanza ili iweze kuendana na wewe.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.