Kumekuwa na kauli na mifano mingi inayoonyesha jinsi ambavyo watu waliofanikiwa zaidi ni wale ambao hawana elimu kubwa. Wakati watu wengi wenye elimu kubwa wakionekana kutokuwa na utajiri mkubwa ukilinganisha na wasiokuwa na elimu kubwa.

Ni kweli kuna mifano ya aina hiyo, lakini kitu kimoja ambacho watu wamekuwa hawakiangalii ni uwezo binafsi wa watu kwenye kupata mafanikio na utajiri mkubwa.

Kuna mifano ya mabilionea wakubwa duniani ambao waliachana na elimu ya chuo ili kwenda kujenga biashara zao. Mfano maarufu ni mwanzilishi wa mtandao wa Facebook, Mark Zuckerberg. Lakini mifano hii imekuwa haiangalii uwezo wa mtu, kwa mfano mtu kama Zuckerberg aliacha chuo kikuu cha Havard, moja ya vyuo bora sana duniani. Mpaka mtu apate nafasi kwenye chuo hicho, lazima awe na uwezo mkubwa sana.

Kwa hiyo basi, ili kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha, lazima mtu awe na uwezo mkubwa pia. Hiyo ni kwa sababu safari nzima ya kujenga utajiri ina vikwazo na changamoto za kila aina ambazo mtu lazima awe imara sana kuzivuka. Lakini pia kujenga utajiri ambao utadumu, lazima misingi yake iwe imara sana.

Tukianza na uwezo, kila mtu anao ndani yake, japo haufanani. Lakini kila mtu kuna vitu ambavyo anaweza kuvifanya vizuri kuliko wengine. Hapo ndipo mtu anakuwa na fursa ya kufanya makubwa zaidi.

Tatizo kubwa ni kwamba uwezo mkubwa ulio ndani ya watu wengi umedumaa. Kwa sababu wao wenyewe hawajui kama wana uwezo fulani na wale wanaowazunguka pia hawajui, kinachotokea ni uwezo huo unakuwa umelala tu ndani yao.

Moja ya vitu ambavyo vinaweza kuamsha uwezo uliolala ndani ya mtu ni kupata elimu, iwe rasmi au siyo rasmi. Kwa elimu rasmi, mtu kukaa kwenye mfumo wa elimu na kupewa changamoto mbalimbali inamsukuma kutumia uwezo wake wa ndani.

Na kwa elimu isiyokuwa rasmi, kwa watu kujisomea vitabu na kupata mafunzo mengine inawafungua sana kufikia na kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yao. Hivyo ndivyo elimu inavyokuwa na mchango kwenye kujenga utajiri mkubwa.

Sasa turudi kwenye uhalisia, kwamba watu wengi waliosoma bado wanashindwa kupata mafanikio na utajiri mkubwa. Hilo ni kweli na ni kwa sababu licha ya kupata elimu, wameshindwa kuitumia vizuri kufikia na kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yao.

Ukweli ni kwamba elimu siyo inayompa mtu mafanikio, bali ni ufunguo ambao unamwezesha mtu kuyaendea mafanikio bila ya kujizuia yeye mwenyewe. Hivyo kila mtu anayetaka mafanikio makubwa, hana budi kujijengea uwezo mkubwa sana kwa kupata kila aina ya elimu anayoweza kupata, hasa ya kusoma vitabu.

Tukirudi kwa wale ambao hawajapata elimu kubwa, wala hawasomi vitabu, ila wanakuwa wamejenga mafanikio na utajiri, je wanakuwa wamevuka hitaji hilo? Jibu ni hapana, kwa uwezo wanaokuwa nao, wanakuwa wameweza kupiga hatua ambazo wamepiga, lakini wanafikia ukomo ambapo hawawezi kukua zaidi ya hapo. Hawa ndiyo ambao huwa wanajenga utajiri, lakini baada ya muda wanaanguka. Na mbaya zaidi ni wakianguka huwa hawawezi kunyanyuka tena, wanakuwa ndiyo wamepotea moja kwa moja.

Wengine wanakuwa wamejenga utajiri ambao wanaweza kudumu nao kwenye kipindi cha uhai wao, kwa sababu ya juhudi wanazoendelea kuweka. Lakini pale wanapofariki, utajiri mkubwa wanaokuwa wameujenga unapotea wote kabisa. Hiyo inasababishwa na wao kukosa uelewa wa kujenga misingi ambayo itauwezesha utajiri wake kudumu kwa muda mrefu.

Ni muhimu sana mtu kuendelea kujipatia elimu ambayo itafungua uwezo wako mkubwa ili uweze kuutumia kujenga utajiri mkubwa. Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimelifafanua hili vizuri. Karibu usikilize kipindi na kujifunza ili uweze kujenga utajiri mkubwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.