Rafiki yangu mpendwa,

Hivi umewahi kujiuliza kwa nini shamba lisilolimwa bado huota magugu lakini halioti mazao yenye manufaa? Ukitaka kupata mazao unayotaka, lazima ulime, upalilie, uweke mbolea ndiyo uvune. Lakini huhitaji kufanya chochote ili magugu yaote shambani.

Mfano huo halisi kabisa unatuonyesha jinsi ambavyo vitu ambavyo havina manufaa kwetu vinavyokuwa rahisi kupatikana kuliko vile ambavyo vina manufaa.

Tabia ya kuahirisha mambo, au kughairisha kama ambavyo imekuwa inajulikana, imekuwa ni kikwazo kwa watu kufanya makubwa kwenye maisha yao.

Mtu anaweza kupanga vizuri kabisa nini anataka kufanya, lakini unapofika wakati wa kufanya ana ahirisha. Cha kushangaza sasa ni anachofanya pale anapoahirisha hicho muhimu inakuwa ni vitu ambavyo havina umuhimu wowote.

Hapa sasa ndipo unapokuja mfano wa magumu tulioanza nao, kwamba kufanya mambo mazuri, ambayo ndiyo malengo uliyonayo, kunahitaji ufanye kazi kubwa. Lakini kufanya mambo yasiyokuwa na tija, haikuhitaji kazi yoyote, ndiyo maana inakuwa rahisi kuahirisha yale muhimu.

Sasa basi rafiki yangu, ninachotaka wewe ufanye ni kugeuza kibao, utumie hiyo hiyo tabia yako ya kuahirisha kwa manufaa yako. Unachofanya ni kuahirisha yale yote ambayo hayana tija.

Inakuwa hivi, pale unapotaka kufanya kitu, ambacho hakina mchango wowote kwenye malengo yako, unaahirisha. Jiambie utafanya baadaye, au siku nyingine. Halafu huo muda upeleke kwenye kufanya vitu vyenye tija kwako.

Kwa kufanya hivi unakuwa umeigeuza tabia ya kuahirisha mambo kuwa ya manufaa kwako, kwa sababu unaahirisha yale yasiyokuwa na tija na kufanya yenye tija.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza hilo kwa kina na hatua za wewe kuchukua ili uweze kuahirisha yote yasiyokuwa na tija na kupata muda wa kutosha wa kufanya yale yanayokuletea mafanikio makubwa. Karibu uangalie kipindi na kujifunza.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.