Faida ni neno ambalo wafanyabiashara wanapenda kulisikia, lakini pia ndiyo kitu kigumu kwa wengi kukipata. Watu wengi huwa wanaingia kwenye biashara kwa kuangalia nini wanachoweza kuuza, kulingana na mahitaji yaliyopo.
Kuna ambao wanafanikiwa kweli kuuza, tena mauzo makubwa tu, lakini wanakuja kushangaa hawaoni fedha. Kwa kuwa wengi wanaingia kwenye biashara bila ya mafunzo sahihi na kwa kuwa pia wengi hawana utamaduni wa kujifunza, huwa wanashindwa kuelewa iweje wauze sana lakini bado fedha hawazioni.

Kwa kukosa uelewa, wengi hutafuta majibu rahisi na hapo ndipo vitu kama ‘chuma ulete’ vinapoanzia. Kwa kuwa mtu anauza sana, lakini haioni fedha, anaamini kuna namna watu wanamchukulia hizo fedha kimazingara, bila ya yeye mwenyewe kujua.
Biashara nzuri kabisa za wengi zimekufa kwa imani hiyo potofu ya ‘chuma ulete’ wakati sababu halisi ni biashara kushindwa kujiendesha kwa faida. Wafanyabiashara wasiokuwa na uelewa huwa wanadhani mauzo ndiyo kila kitu kwenye biashara. Kwamba kama wakiweza kununua kwa bei ya chini na kuuza kwa bei ya juu, basi wameiweza biashara.
Ni pale wanaponunua kwa bei ya chini na kuuza kwa bei ya chini lakini wasizione fedha ndiyo wanashindwa kuelewa nini kinaendelea. Kinachoendelea ni ukokotoaji wa faida haujulikani na hivyo mfanyabiashara kujiendea na biashara bila kujua kama inaingiza faida au hasara.
Hesabu ya wengi ya faida ni kuchukua mauzo na kutoa manunuzi. Hiyo siyo hesabu sahihi, ni faida tu ya awali. Faida kamili ya biashara ni baada ya kuingiza gharama zote za kuendesha biashara hiyo. Na kwenye gharama za biashara ndipo watu wengi wanapopoteza fedha, tena bila ya kujua, kwa sababu hawana kumbukumbu nzuri wanazoweka kwenye matumizi yao.
Ili kujenga biashara inayoingiza faida kubwa, kuna mambo muhimu sana unayopaswa kuyazingatia.
Moja ni kuhakikisha kumbukumbu zote za mzunguko wa fedha kwenye biashara zinatunzwa vizuri. Kila fedha inayoingia na inayotoka kwenye biashara inapaswa kuwekwa kwenye kumbukumbu. Hapo utaweza kujionea wazi ni wapi fedha za biashara zinapotelea.
Mbili ni kujua hesabu sahihi ya kukokotoa faida kwenye biashara. Huwa kuna hesabu mbili, moja ni faida ghafi ambayo unachukua mauzo kutoa manunuzi. Na ya pili ni faida halisi ambayo unachukua faida ghafi kutoa gharama za kuendesha biashara, ambazo ni tofauti na manunuzi. Kwa biashara nyingi, faida ghafi inaweza kuwepo, lakini faida kamili ikakosekana kutokana na gharama za biashara kuwa kubwa.
Tatu ni kudhibiti gharama za biashara. Kwa sababu tumeona sehemu ya kwanza inayotafuna faida ya biashara ni gharama, hizo zinapaswa kudhibitiwa. Hapa gharama zote zisizokuwa za msingi zinaondolewa na kubaki zile za msingi tu. Gharama huwa zina tabia ya kupanda pale kipato kinapoongezeka. Unapaswa kuzidhibiti ili faida iweze kuonekana.
Nne ni kukuza zaidi mauzo. Kudhibiti gharama ni kitu chenye ukomo, kwa sababu utafika mahali ambapo huwezi kupunguza tena, hasa kwa matumizi ya msingi. Hivyo hatua inayofuata baada ya kudhibiti gharama ni kuongeza sana kipato kwa kukuza zaidi mauzo. Kwa biashara nyingi, faida zake huwa ni ndogo ndogo sana, hivyo ili kubaki na faida baada ya kuweka matumizi, lazima mauzo yanayofanyika yawe makubwa sana. Eneo la kukuza mauzo linapaswa kufanyiwa kazi kwa uhakika ili kubaki na faida nzuri kwenye biashara.
Tano ni kutumia kanuni ya 20/80. Asilimia 80 ya faida inayopatikana kwenye biashara inatokana na asilimia 20 ya vitu vinavyouzwa. Hiyo ina maana kama biashara imepata faida ya laki moja na inauza vitu 10, elfu 80 imechangiwa na vitu viwili tu. Hiyo inaonyesha kuna vitu vichache vyenye faida kubwa na vingi vyenye faida ndogo. Ili kukuza faida, unapaswa kuweka nguvu zaidi kwenye vitu vichache vyenye faida kubwa badala ya vitu vingi vyenye faida ndogo.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA, nimeeleza kwa kina kuhusu haya kwenye kujenga biashara inayoingiza faida kubwa. Karibu usikilize kipindi na kwenda kuchukua hatua ili upate faida nzuri kwenye biashara yoyote unayofanya.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.