Mteja Shabiki

Shabiki ni mtu anayependa sana kitu. Wengi wetu tunaposikia neno shabiki, akili yetu inatupeleka moja kwa moja michezoni. Maana, ni sehemu neno shabiki hutumika sana. Utasikia Derrick ni shabiki wa Simba. Amos ni shabiki wa Yanga. Anna ni mshabiki wa mpira wa wavu au tenisi kadhalika na maeneo mengine.

Ushabiki unamaanisha yale mapenzi anayokuwa nayo mtu kwenye kitu fulani. Anakuwa tayari kuweza kutetea kitu hicho hadi mwisho. Ndiyo maana, mashabiki wa mpira wa miguu wakikaa sehemu hata ugomvi unaweza kutokea ikiwa utaiongelea vibaya timu yake au wachezaji wake. Ila hatusikia Rwekaza ni shabiki wa Amka Consultants au Hamasika Consultants au Winner Motorcycle, KIU kwa sababu hatujaelekezwa.

Kwenye mauzo shabiki ni mteja ambaye amevuka hatua zote na mwenye ufahamu mkubwa kuhusu biashara yako.

Ni mtu anayejua biashara yako nje ndani na humwambii kitu kuhusu biashara yako. Ni mteja ambaye hachukui mahali pengine popote isipokuwa kwako. Ikitokea ukafunga biashara au kupata changamoto anakuwa tayari kukusubiri. Hii ni kutokana na uaminifu anaokuwa amejenga kwenye biashara yako. Sio mteja anayeruka ruka au kubabaisha. Anakuwa na uaminifu mkubwa na biashara yako. Huyu ni zaidi ya rafiki.

Hivyo, kama mtu wa mauzo unahitaji kutengeneza mashabiki wengi kwenye huduma yako. Hawa ni wateja wanaokuwa nawe katika nyakati zote. Wanaweza kuwaambia wengine kuja kwako, kuwaelezea au kuwaleta kwenye biashara yako. Maana wanakuwa na taarifa nyingi kuhusu wewe na utendaji wako. Ni kazi kwako kuweka juhudi na uaminifu mkubwa kuwatengeneza.

Kama tulivyoona hapo juu kwamba shabiki ni mtu anayependa sana kitu ndivyo tunavyotaka na sisi kutengeneza wateja mashabiki. Wateja wanaopenda biashara zetu. Wateja ambao hawapo tayari kuona mtu yeyote anaiongelea vibaya biashara yetu. Wateja wenye utayari wa kukutetea mahali popote wanapokuwa.

Kwenye ngazi za wateja hii ndiyo ngazi ya mwisho kabisa. Sio ngazi au aina ya wateja unaowatengeza siku moja au wiki moja. Inahitaji muda mrefu. Hapa kama ni ndiyo tayari inafungwa kabisa. Mtu anakuwa hana wasiwasi kuhusiana na wewe. Anakujua zaidi ya asilimia 90, anakuwa amefanya manunuzi mengi sana.

Sio kila mteja anaweza kuifikia hatua hii, hili lazima ulijue. Maana ni wateja ambao hata kiwago cha manunuzi yao kinakuwa ni kikubwa kulinganisha na wateja wadogo. Ni mteja anayehitaji uwekeze nguvu kubwa kumpandisha.

Gharama za kumrudisha mteja shabiki ni mara kumi ya kumtafuta mteja lengwa. Maana anakuwa ameamini biashara yako kwa kiwago cha hali ya juu. Hivyo, unapokuwa umemfanyia kitu ambacho hakiwezi kuvumilika akawa ameondoka, kazi isiyo ya kawaida inahitajika kujenga imani yake. Ndiyo maana nikasema, huyu anahitaji “special treatment”.

Sifa kuu za mteja shabiki;
Moja; Ni kuitetea biashara yako. Kama ilivyo upande wa mpira wa miguu. Shabiki wa ukweli wa timu huwa anaitetea vema. Inapotokea timu yake imefungwa anasikitika na kuumia, wengine huenda mbali na kushindwa kula kwa sababu ya mapenzi wanayokuwa nayo katika timu hiyo.

Mbili; Ni mteja anayeelewa changamoto zako.
Inapotokea changamoto katika biashara yako, yupo tayari kuingia mfukoni mwake kukusaidia ili utatue changamoto yako. Maana biashara yako inakuwa inamtegemea na yeye anakuwa anaitegemea. Sio mteja anayependa kuona ukipata changamoto nyingi.

Tatu; Anahitaji kuthaminiwa kwa kiwango cha hali ya juu.
Wakati mwingine anahitaji kuhusishwa katika baadhi ya mambo ambayo biashara yako inafanya.

Jinsi ya kutengeneza wateja shabiki;

Moja; Wape huduma bora zaidi ya matarajio yao.
Mbili; Jali maslahi yao.
Tatu; Washirikishe katika baadhi ya mambo.
Nne; Mfanye ajione ni Mfalme.
Tano; Kuwa na orodha ya wateja shabiki. Angalau kila wiki waguswe mara moja.

Kumbuka, hii ni hatua kubwa inayohitaji kampuni kuweka muda mwingi katika kuwahudumia wateja wake hadi kufika kiwango cha juu. Kulifanikisha hilo wape sababu za wao kuendelea kununua kwako.

Maswali ya kujiuliza;
Je, biashara yako ina wateja shabiki wangapi?
Kwanini ananunua?
Kwanini ananunua kwetu?

Maswali hayo yatakusaidia kupata majibu na nzuri kuendelea kuwaweka karibu na wateja wako.

Fanyia kazi yote uliyojifunza hapa.

Imeandaliwa na Lackius Robert, Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo na Mwandishi. Tuwasiliane 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz