3327; Msingi usipokuwa sahihi.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye ujenzi wa kitu chochote kile, msingi huwa ndiyo eneo muhimu zaidi.
Ni uimara wa msingi ndiyo ufakaoamua ni kitu kikubwa kiasi gani kinachoweza kujengwa juu yake.
Kwa bahati mbaya sana, msingi usipokuwa sahihi, huwa ni vigumu sana kuja kuubadili au kuuboresha baadaye.
Kujaribu kufanya hivyo kuna hatari ya kuharibu kila kilichojengwa na kuishia kubaki na kitu ambacho ni dhaifu kuliko ilivyokuwa awali.
Hivyo msingi ni eneo muhimu la kuweka uzito wakati wa kujenga kitu chochote kile.
Ni muhimu sana msingi uwe sahihi, ili mengine yanayofuata yaweze kuwa sahihi pia.
Hili ni kuanzia kwenye majengo, mifumo na hata maisha binafsi.
Kinachopelekea wengi kushindwa au kupata anguko baada ya mafanikio ni udhaifu wa misingi wanayokuwa wamejenga.
Wanakuwa wanataka mafanikio makubwa, lakini msingi walioanza nao unakuwa siyo sahihi.
Hivyo hilo pekee linazuia mafanikio yasipatikane. Na hata yakipatikana, yanakuwa dhaifu sana kiasi cha kuwa rahisi kuanguka.
Kwenye KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, mambo yote tunayafanya kwa kuangalia misingi iliyopo.
Tunayo misingi inayotuongoza kwenye mambo yetu yote na huwa tunahakikisha tunaizingatia misingi hiyo kwenye kila maamuzi tunayofanya.
Kuwa ndani ya jamii hii ya KISIMA CHA MAARIFA ni kuchagua kuizingatia na kuiishi misingi hiyo kwenye kila eneo la maisha yako.
Ni kuhakikisha unaanza na misingi sahihi kwenye kila jambo kabla ya kulikuza zaidi.
Ukuaji ni sahihi na rahisi pale misingi inapokuwa sahihi.
Mara zote zingatia misingi yote iliyopo sahihi ili kujenga kitu sahihi na kitakachokupa yote unayoyataka.
Na pale unapokuja kugundua baadaye kuna kitu umekijenga bila ya misingi sahihi, anza kukifanya upya kwa hiyo misingi iliyo sahihi.
Kujaribu kurekebisha misingi isiyo sahihi ni kupoteza muda na nguvu kwa jambo ambalo mwisho wa siku litaishia vibaya.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe