Rafiki yangu mpendwa,
Huwa kuna kauli inasema mapenzi yanaendesha dunia. Wengi hutumia kauli hiyo kwenye mahusiano ya mapenzi, lakini ni kauli ambayo ina ukweli kwenye upendo kama nguvu kuu inayoendesha dunia.
Pamoja na changamoto nyingi ambazo zipo duniani, bado upendo ni moja ya nguvu kuu zinazoiendesha dunia. Hiyo ni kwa sababu watu huwa wanasukumwa zaidi pale wanapokuwa na upendo juu ya kitu fulani.
Hata pale unapomwona mtu anafanya jambo ambalo ni la kijinga, ukichunguza kwa ndani, kuna namna ambavyo upendo unakuwa umehusika. Upendo unaweza kumpa mtu nguvu ya kufanya ambayo asingeweza kufanya bila ya kuwa na upendo huo.

Na hata nguvu nyingine ambazo zinaendesha dunia, ni pale upendo unaposhindikana. Kwa mfano hofu ambayo ni nguvu nyingine, huwa inapata nafasi pale upendo unapokosekana. Wengi hudhani kinyume cha upendo ni chuki, lakini ukweli ni kinyume cha upendo ni hofu. Mtu anapokuwa na upendo, hofu inakosa nafasi kabisa.
Nguvu nyingine inayoendesha dunia ni wivu, watu huwa wanasukumwa sana kufanya vitu kutokana na wivu. Na ukiangalia wivu kwa undani, ni upendo ambao umekosewa. Ni upendo ambao umeenda zaidi upande wa ubinafsi. Mtu anakuwa na wivu pale anapokuwa na upendo wenye ubinafsi, kuona yeye anastahili zaidi kuliko wengine.
Japo watu huwa wanasema kuna wivu mzuri na wivu mbaya, kikubwa ni wivu una msukumo kwa watu na wivu huo ni pale upendo unapokuwa kwa ubinafsi.
Sasa tumeshaona jinsi ambavyo upendo ni nguvu kuu inayoendesha dunia, kinachofuata ni jinsi ya kuitumia nguvu hii kufanya makubwa kwenye maisha yako.
Zipo ngazi tatu za kutumia nguvu ya upendo kuweza kufanya makubwa kwenye maisha yako.
Ngazi ya kwanza ni kujipenda sana wewe mwenyewe.
Jipende wewe mwenyewe, jikubali sana vile ulivyo. Usitamani ungekuwa tofauti kwa namna yoyote ile. Vile ulivyo na mapungufu yako, ndivyo ulivyo na hivyo hivyo unaweza kufanya makubwa. Wengi sana wanashindwa kufanya makubwa kwa sababu hawajipendi wala kujikubali. Wanatamani wangekuwa tofauti na vile walivyo, kitu ambacho hakiwezi kutokea kama mtu hatajipenda na kujikubali kwanza. Anzia hapo kwenye kujipenda wewe mwenyewe kama unataka kufanya makubwa kwenye maisha yako.
SOMA; 1830; Upendo Wa Kweli…
Ngazi ya pili ni kuwapenda watu wote wanaokuzunguka.
Wapende watu wote wanaokuzunguka na kuwakubali vile walivyo. Usitake watu wawe kama vile unavyotaka, bali waache wawe vile walivyo. Shirikiana na wale ambao unaweza kuendana nao kwenye yale unayofanya au unayosimamia. Heshimu wale ambao mnatofautiana na waache waendelee na mambo yao. Usiwe na chuki na mtu yeyote, hata kama amekufanyia nini. Sambaza upendo kwa watu wote, kwa nia njema kabisa na utaweza kushirikiana na watu sahihi kufanya makubwa. Huwezi kufanya makubwa peke yako, unahitaji watu wengi wa kushirikiana nao, kwa kuwapenda watu, utaweza kupata wengi sahihi wa kushirikiana nao.
Ngazi ya tatu ni kupenda kile unachofanya.
Unapochagua kufanya kitu chochote kile, basi hakikisha unakipenda kweli. Hakikisha kinatoka ndani yako kweli na kifanye kwa moyo mmoja. Weka kila ulichonacho kwenye kufanya kitu hicho kwa viwango vya juu sana. Usifanye kitu chochote kwa juu juu kwa sababu unaona unakifanya kwa muda mfupi tu. Kila unachoruhusu mikono yako ishike, kiache kikiwa bora zaidi. Acha alama ambayo watu wengine watajua ni wewe uligusa kitu hicho. Ni mapenzi ya dhati kwenye kitu unachofanya ndiyo yatakusukuma uendelee kufanya licha ya kukutana na magumu na changamoto zinazowakatisha wengi tamaa.
Jenga upendo kwenye maeneo hayo matatu ya maisha yako, jipende wewe mwenyewe, wapende wengine na penda kila unachofanya. Kwa kufanya hivyo, nguvu ya upendo ambayo ndiyo inaendesha dunia, itakuwezesha kufanya makubwa kwenye maisha yako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.