
Miadi ni ahadi ya kukutana au kuongea na mtu katika muda maalumu na kuhusu jambo fulani. Miadi ni makubaliano ya pande zote mbili kuongelea mada fulani. Mfano, Juma na Peter wamepeana miadi wakutane ofisini kesho asubuhi.
Kabla hujauza kile ambacho unawataka wateja wanunue, kuna kitu muhimu ambacho unapaswa kukiuza kwanza kwa wateja wako. Kitu hicho ni ushawishi wa mteja akubali ni kukutana au kuongea na wewe. Hapo ndipo suala la miadi linapopata nafasi kama nilivyoelezea juu.
Hivyo ushawishi wa kwanza unaopaswa kuwa nao ni wa kuwafanya wateja wawe tayari kukutana na wewe. Njia nzuri ya kuwashawishi wateja kukutana nao ili uweze kuwaeleza kuhusu kile unachouza ni kuweka miadi. Watu wana mambo mengi ambayo tayari yanaendelea kwenye maisha yako. Hivyo siyo rahisi kuwapata wakati wowote unapotaka kuwafikia.
Kwa kuomba miadi ya kukutana na mtu na akakubali mkutane kwenye muda fulani, inakuwa vizuri zaidi kuliko kukutana na mtu bila miadi. Unapokutana na mteja kwa miadi kwanza anaona unaheshimu muda wake ndiyo maana umeweka miadi. Na pili anakuwa tayari kukusikiliza maana alitenga muda huo wa miadi, tofauti na ungekutana naye akiwa na majukumu mengine.
Ni muhimu kuweka miadi kabla ya kukutana na wateja na pale unapowatembelea bila ya miadi omba kwanza nafasi ya mazungumzo badala ya kwenda kwenye mazungumzo moja kwa moja.
Aina za miadi;
Moja; Ana kwa ana
Hapa unakutana na mtu kisha uso kwa uso na kuanza kuzungumza naye. Hii ndiyo aina kuu ya miadi na wengi wetu tumezoea aina hii ya miadi.
Mbili; Simu.
Ni aina ya miadi unayopewa na mtu aliye mbali au unayeshindwa kumuona ana kwa ana kutokana na sababu za hapa na pale. Aina hii ya miadi wengi wetu hatujaizoea. Mtu anapotwambia hana muda, tunasubiria apate muda na baadhi yetu kuacha.
Hapa kuna misingi mikuu miwili ya kusimamia mara zote
- Kwanza uza miadi.
- Kisha ndiyo uuze bidhaa yako
Mambo muhimu wakati wa kuomba miadi;
Moja; Siku.
Unapoomba miadi, hakikisha unajua siku ya kukutana au kuwasiliana na mhusika.
Pili; Muda.
Baada ya kujua siku husika, ni muhimu pia kujua muda ili ujiandae vema.
Tatu; Mahali.
Kama ni miadi ya kukutana na mtu, hakikisha eneo husika mtakapokutana unalijua. Hii inasaidia kufika mapema eneo kwa wakati.
Nne; Mada ya mazungumzo.
Nini mnaenda kuzungumzia ni muhimu pia kujulikana, ili maandalizi yawepo.
Muhimu; Unapopata miadi, usionekane muuzaji. Kwa sababu hakuna kitu ambacho watu wanakikwepa kama kukutana na watu wa mauzo. Maana tayari wana mtazamo mbaya kwa watu wa mauzo.
Kwenye kuomba miadi, mwonyeshe mteja unaenda kujadiliana naye kitu ambacho kina manufaa kwake. Mwonyeshe una kitu ambacho kinaweza kumsaidia kutatua matatizo aliyonayo au kumpatia mahitaji yake.
Uzuri ni kwamba kila mtu kuna kitu anahitaji au kuna tatizo anataka kutatua. Ukijua hayo na mazungumzo yako yakajikita hapo, utapewa nafasi ya kusikilizwa na hapo kuwa na fursa ya kuweza kumshawishi mtu anunue kile unachouza. Lakini kwanza ni baada ya kuwa umemshawishi akusikilize, kwa kuongelea yale yenye manufaa kwake.
Baada ya kupata miadi zingatia yafuatayo;
Moja; Jitambulishe.
Ni kitu muhimu sana baada ya kukutana na mhusika. Inaweza kuwa salamu au majina kama ni mgeni kwako. Hii inasaidia kujua vema unayezungumza naye.
Mbili; Lengo.
Hakuna mazungumzo yasiyo na lengo. Hili lazima ulijue na kulifayia kazi. Baada ya kujitambulisha nenda kwenye lengo. Mwambie lengo la kukutana na wewe ni ….
Tatu; Sikiliza.
Eneo muhimu kuweka nguvu kwenye mazungumzo ni kuwa mskilizaji mzuri zaidi ya muongeaji. Hii itakusaidia kuelewa vema unayezungumza naye.
Nne; Uliza maswali.
Hata kama miadi umeomba wewe, usiache kuuliza maswali. Uzuri wa maswali ni kupewa majibu, unapouliza unapata uelewa zaidi juu ya mada ya mazungumzo.
Tano; Hitimisho.
Kama kuna kitu cha kumuonyesha, muonyeshe. Kisha mshukuru unayezungumza naye. Mpe hatua za kuchukua. Kama ni kupata miadi mingine au kulipia ikiwa kuna nafasi fanya hivyo.
Faida Za Miadi;
Moja; Kuokoa muda.
Kwa kuwa na mpango wa nani unakutana naye na wakati gani, inasaidia kufanya mambo mengine badala ya kuhofia mara zote kuhusu nani utakutana naye.
Mbili; Thamani kubwa.
Kwa kuomba miadi kwa mteja, mnapokutana anaona umempatia thamani kubwa hasa ya muda.
Tatu; Ushawishi.
Huwezi kuuza bila ya kufanya mazungumzo na mteja, na ili uweze kufanya naye mazungumzo, lazima akubali kukupa miadi. Unapopewa miadi, unapata uwezo wa kumshawishi mteja.
Nne; Umakini.
Kuwa na miadi kunamfanya muuzaji afanye kazi kwa umakini badala ya kwenda tu kwa mazoea. Unajiandaa vizuri kabla ya kukutana na mteja, kwa sababu tayari unajua siku na muda mnaokwenda kukutana.
Kazi yako ya kwanza kama muuzaji ni kumshawishi mteja akubali muongee au mkutane na mkishakutana ndiyo mengine yaendelee.
Hivyo mara zote kuwa na maandalizi mazuri kabla hujamwomba mtu miadi, ili uweze kumshawishi akubaliane na wewe.
Fanyia kazi yake yote uliyojifunza katika somo hili.
Imeandaliwa na Lackius Robert Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo. Tuwasiliane 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz.