Rafiki yangu mpendwa,

Kwa zama tunazoishi sasa, kuanzisha biashara imekuwa ni kitu rahisi sana. Kwani hata mtu asiye na mtaji au sehemu ya kufanyia biashara, bado anaweza kuanzisha biashara kwa kutumia tu simu yake na akiwa nyumbani kwake.

Pamoja na urahisi huo wa kila mtu kuweza kuingia kwenye biashara, biashara zinazopata mafanikio makubwa zimekuwa ni chache sana. Biashara nyingi zinazoanzishwa huwa zinakufa ndani ya mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake. Na hata zile ambazo hazifi, huwa zinadumaa, hazikui licha ya kuwepo kwa muda mrefu.

Kinachopelekea hali ya biashara nyingi kushindwa kukua ni kile kile ambacho kimekuwa kinafanya kuingia kwenye biashara kuwa rahisi. Kuanza biashara imekuwa ni rahisi kwa sababu ya urahisi wa kuiga yale ambayo tayari wengine wanafanya. Mtu anapoona biashara nyingine yenye mafanikio na yeye anaenda kuanzisha biashara kama hiyo.

Kujenga biashara zenye mafanikio imekuwa ni kitu kigumu kwa sababu hiyo hiyo ya kuiga. Kwa sababu biashara za kuigana zinafanana, zimekuwa zinakabiliana na ushindani mkali sokoni. Ushindani huo unapelekea bei kushuka sana na faida kuwa ndogo. Hakuna biashara inayoweza kuwa na mafanikio makubwa kama inaingiza faida ndogo.

Bilionea Peter Thiel kwenye kitabu chake kinachoitwa ZERO TO ONE, ameeleza kwa kina hali hii ya biashara za kuigana kuwa na ushindani mkali sokoni na zote kuishia kupoteza. Ili kuondokana na hilo, kwenye kitabu chake ameonyesha njia pekee ya kuchukua ni kujenga biashara zinazohodhi soko (monopoly). Anasema hivyo ndivyo mtu anaweza kujenga biashara yenye mafanikio makubwa.

Lakini sasa, kuna mtego hapo, kuhodhi soko ni kosa kisheria. Sheria za biashara na uchumi zinataka kuwepo na ushindani sawa sokoni ili kusiwe na ulanguaji au bei za kuumiza. Je Thiel anataka tuvunje sheria ili kujenga biashara zenye mafanikio? Jibu ni hapana, badala yake ametupa mpango mzuri wa kujenga biashara zinazohodhi soko bila kuvunja sheria.

Kitu cha kwanza kabisa ambacho anatutaka tufanye ni turudi kwenye ugunduzi wa teknolojia mpya ambazo zinaleta kitu kipya kabisa kwenye soko. Ushindani mkali unatokana na kuiga kile ambacho tayari kipo sokoni, Thiel anaita hilo ni utandawazi. Kuhodhi soko kunahitaji ugunduzi wa kitu kipya kabisa ambacho hakipo sokoni, Thiel anaita hilo ni teknolojia.

Hivyo basi, msingi wa kwanza wa kujenga biashara ambayo itakuwa na mafanikio makubwa kupitia kuhodhi soko ni kuwa na teknolojia. Uzuri ni kwamba, serikali inaweza kukupa kibali cha kuhodhi soko pale unapogundua kitu kipya, kwa kukupa hatimiliki ya ugunduzi wako kiasi kwamba hakuna mwingine anayeweza kuutumia bila ruhusa yako.

Msingi mwingine ambao Thiel ameshirikisha kwenye kitabu chake ni kuwa na ukuaji mkubwa wa kibiashara ambao unapunguza bei na hivyo kuleta nguvu kubwa sokoni. Pale biashara inapokuwa na ukuaji mkubwa, gharama za uendeshaji zinapungua kwa kulinganisha na uzalishaji wake. Hilo linapelekea kuiwezesha biashara kuhodhi soko na kuzuia washindani wasiweze kuingia kwenye soko hilo.

Ushindani wowote unaojaribu kuingia kwenye soko ambalo biashara imelishika kwa nafasi kubwa, unashindwa kwa sababu ya gharama kwa washindani inakuwa kubwa kuliko kwa biashara iliyohodhi.

Hii ni misingi miwili kati ya minne ambayo Thiel ameielezea kwenye kitabu hicho cha ZERO TO ONE. Misingi mingine miwili nimeielezea kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambacho nimeshirikisha mengi zaidi kutoka kwenye kitabu hicho. Karibu usikilize kipindi, ujifunze na kwenda kujenga biashara yenye nguvu ya kuhodhi soko na kukupa mafanikio makubwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.