Rafiki yangu mpendwa,

Tangu enzi na enzi, watu wamekuwa wanatafuta njia ya mkato ya kupata mafanikio makubwa, ambayo haihitaji mtu kufanya kazi au kusubiri kwa muda mrefu.

Lakini katika nyakati zote, haijawahi kuwepo njia hiyo, zaidi ya watu kupoteza muda, nguvu na hata wakati mwingine fedha.

Mfano mmoja ambao ulikuwa maarufu sana na ambao umewahi kuwaponza hata watu waliokuwa na akili sana kama mwanasayansi Isaac Newton ni kugeuza chuma/risasi kuwa dhahabu.

Kwa miaka mingi kulikuwepo na hiyo imani kwamba kuna mchanganyiko ambao ukichanganywa kwa usahihi na kuwekwa kwenye madini ya chuma au risasi basi yangeweza kugeuka kuwa madini ya dhahabu.

Watu walitumia muda na gharama kubwa sana kutafuta huo mchanganyiko ambao ungeweza kukamilisha hilo, maana waliona ndiyo njia ya mkato ya kupata utajiri mkubwa.

Hata mwanasayansi Isaac Newton, ambaye alikuwa mmoja wa watu wenye akili sana, naye aliingia kwenye huo mtego. Inaelezwa kwamba alitumia sehemu kubwa ya muda wake kutafuta huo mchanganyiko.

Kwa uelewa tulionao sasa kuhusu madini, tunaweza kuwacheka watu hao wa zama zilizopita kwa kuamini kitu cha ajabu kiasi hicho. Lakini tukianza kuangalia yale yanayoangaliwa na wengi kama njia za mkato kwa sasa, kicheko kitakuwa ni kile kile.

Watu wengi wanacheza michezo ya kubahatisha na kamari wakiamini ni njia ya mkato kwao kupata utajiri mkubwa. Lakini ni wachache sana wanaoshinda michezo hiyo na hata hao wanaoshinda, hawapati utajiri waliokuwa wanategemea kuupata. Kwani hata wakipata fedha nyingi kiasi gani, wanaishia kupoteza zote.

Kumekuwa pia na aina mbalimbali za uwekezaji ambazo zinakuja, zikiwaahidi watu kukuza uwekezaji wao ndani ya muda mfupi. Lakini matokeo yake imekuwa ni watu kupoteza uwekezaji wanaokuwa wamefanya.

Haya yote yanatuonyesha jinsi ambavyo njia za mkato za kupata mafanikio hazipo, kwani zote ambazo zimejaribiwa, zimeishia kuwaumiza watu.

Lakini ipo njia moja ambayo nakwenda kukushirikisha hapa, ambayo ukiifanyia kazi utaweza kupata matokeo makubwa sana.

Tahadhari kuhusu njia hii ni kwamba itakuhitaji uweke kazi na pia itakuhitaji muda. Sasa unaweza kusema inakuwaje njia ya mkato kama bado mtu unaweka kazi na muda. Usiwe na shaka, twende pamoja na utaona.

Abraham Lincoln aliwahi kunukuliwa akisema; ‘ukinipa masaa 6 ya kukata mti, nitatumia masaa 6 kunoa shoka langu.’ Twende taratibu na hii kauli, ana masaa 6 ya kukata mtu, ambayo yote atayatumia, kwa hiyo hakuna kufupisha muda. Lakini kwenye matumizi ya muda huo, masaa 4 ni ya kunoa shoka na masaa 2 ya kukata. Hivyo bado pia atakata mti, hivyo kazi lazima iwekwe.

SOMA; Vitu Vitatu (03) Unavyohitaji Ili Unufaike Na Usomaji Wa Vitabu.

Swali ni mtu anakuwa ameokoa nini hapo? Jibu ni amepunguza nguvu na muda ambao anatumia kupata kile anachotaka. Na hiyo ndiyo inatupeleka kwenye njia pekee ya mkato inayoweza kukupa mafanikio makubwa unayoyataka.

Njia ya mkato, ambayo ni ya uhakika kwako kupata mafanikio makubwa ni kujifunza kupitia usomaji wa vitabu. Vitu vingi ambavyo unafanya, tayari wengine wameshavifanya. Makosa unayofanya, wengine walishayafanya huko nyuma. Vikwazo vinavyokuzuia sasa, wapo wengine ambao walikutana navyo pia.

Kwa bahati nzuri sana, wengine hao walikaa chini na kuandika uzoefu wao kwenye safari zao za mafanikio na kugeuza kuwa vitabu. Kwa wewe kusoma kitabu kimoja, tena kwa masaa machache, unakuwa umepata uzoefu wa mtu wa miaka 30.

Je huoni hiyo ni njia ya mkato? Badala ya kurudia makosa ambayo wengine wameshayafanya, badala ya kuzuiwa na vikwazo ambavyo wengine wameshavivuka, wewe unakwenda moja kwa moja kwenye yale ambayo yanafanya kazi.

Hivyo ndivyo kujifunza kupitia usomaji wa vitabu kunavyokuwa njia ya mkato kwako kufanikiwa.

Hatua ya wewe kuchukua ni kujua nini hasa unachotaka na nini kinakuzuia kukipata. Kisha chagua vitabu bora vilivyoandika kuhusu kitu hicho na visome kwa kina. Kisha weka mkakati wa yale utakayofanya na utakayoacha kufanya na uufuate mkakati huo. Utapunguza muda, nguvu na fedha ambazo ungepoteza kama usingekuwa na miongozo hiyo.

Huwa inanishangaza sana unakuwa mtu anaenda kuanzisha biashara ya mtaji wa Milioni 10, lakini hayupo tayari kutenga masaa 10 ya kusoma kitabu cha biashara ambacho anaweza kununua kwa shilingi elfu 10. Atasema hana muda, ni fedha nyingi kwa kitabu na tayari anajua kila kitu. Lakini pale anapoingia kwenye biashara, anafanya makosa ambayo angeweza kuyaepuka kama angesoma kitabu na kuzingatia.

Rafiki, usiwe kama wengi ambao wanapoteza kwa kushindwa kunufaika na njia hii ya mkato na ya uhakika ya kuweza kufanya makubwa. Soma vitabu, pata maarifa na yatumie kupata kile unachotaka.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.